MKUU wa wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Mwanahamisi Munkunda amewataka wawekezaji kwenda kuwekeza katika wilaya hiyo kwani tatizo la maji ambalo lilikuwa kero kwao limeshapatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Alitoa kauli hiyo jana alipofanya kikao na Wadau wa maji na menejimenti ya Mamlaka ya Maji Same Mwanga (Samwasa) mara baada ya kutembelea na kujionea mradi wa maji Mwanga - Same - Korogwe ambao awamu ya kwanza imeshakamilika na maji yanatoka katika wilaya ya Mwanga na Same.
Alisema kuwa, awali wawekezaji walikuwa wakishindwa kuwekeza katika wilaya hiyo kutokana na tatizo la maji lakini kwa sasa kupitia serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweza kukamilisha mradi huo.
"Tunatambua wawekezaji wengi walikuwa wakikataa kuja kuwekeza katika wilaya yetu kutokana na tatizo la maji tulilokuwa nalo lakini serikali imeonyesha kwa vitendo kuondoa changamoto zinazowakabili wananchi wake ambapo kwa sasa tunapata maji masaa 24" Alisema Mwanahamisi.
Alisema kuwa, mradi huo umeliliwa na wananchi kwa muda mrefu lakini Dkt. Samia amekuja kuumaliza na kutatua kiu ya Wanamwanga ambapo kwa sasa wanayo maji ya kutosha.
Mkuu huyo alidai kuwa, lengo la mradi huo ni kuifungua wilaya ya Mwanga kiuchumi na kimaendeleo na kuwataka kuwa walinzi wa mradi huo ili uweze kudumu muda mrefu.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya amewataka Watumishi wa Mamlaka ya maji Samwasa kubadilisha utendaji kazi na kuachana kufanya kazi kwa mazoea ili lengo la serikali na kuwahudumia wananchi wake liweze kutimia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji Samwasa, Mhandisi Rashid Mwinjuma alisema kuwa, uhitaji wa maji kwa wilaya ya Mwanga na Same ni lita za ujazo milioni 8 kwa siku huku mradi huo ukiweza kuzalisha lita za ujazo milioni 55.5 kwa siku hivyo maji yapo ya kutosha.
Mhandisi Mwinjuma alisema kuwa, kwa sasa Mamlaka hiyo inazidai taasisi za serikali na watu binafsi milioni 149.23 kwa Mwanga na milioni 132.22 kwa Same ambapo amehimiza wananchi kuendelea kulipa Ankara zao pamoja na madeni.
Alisema kuwa, kwa sasa Mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto ya uchelewaji wa vifaa kama mabomba kea ajili ya maunganisho ya maji kwenye mtandao wa mradi, uhaba wa fedha inayopelekea kutomudu gharama za ujenzi wa miradi na uendeshaji.
"T inakabiliwa na changamoto ya baadhi ya wateja kutolipa Ankara zao kwa wakati ambapo kwa sasa tunadai zaidi ya milioni 281 lakini pia upotevu wa maji mkubwa kutokana na uchakavu wa miundombinu" Alisema Mhandisi Mwinjuma.

MKUU wa wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ameliagiza Jeshi la polisi kufanya msako na kuwakamata watu watatu wa familia moja wanaotuhumiwa na kwa maua ya Mwenyekiti wa kitongoji cha Kampimbi kata ya Ndungu, Charles Johnson Mkuruto(58).
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya, mnamo Aprili 26 mwaka huu majira ya saa tano na nusu asubuhi huko kitongoji cha Kampimbi kijiji cha Ndungu kata ya Ndungu mtu mmoja aitwae Johnson Mkuruto(58) Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sinangoa 'A' aliuwawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu ya kichwani na nyuma ya bega la kulia.
Alisema kuwa, Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Ardhi kata ya Ndungu alikatwa na watu watatu ambao aliwataja kwa majina kuwa ni Mohamad Makundi, Hamad Makundi na Mnandi Makundi na kutoweka kusikojulikana.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, sababu ya mauaji hayo ni mgogoro wa Ardhi uliopo Mahakama ya Ardhi ya Ndungu.
"Baraza la Ardhi jana lilienda eneo la mashamba yanayobishaniwa ndipo watuhumiwa walimvamia marehemu na kumkatakata na kitu chenye ncha kali kisha kukimbia" Alisema Kasilda.
Na Elizabeth Joseph, Monduli.
WANANCHI wilayani Monduli wameshauriwa kuhakikisha wanatumia Mfumo mpya wa ukusanyaji Mapato ya ndani ya Halmashauri (TAUSI) ili kuongeza ufanisi kwenye ukusanyaji wa mapato.
Ushauri huo umetolewa na Ofisa biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Bw,Abdallah Magambo wakati wa mahojiano na chombo hiki kuhusu mfumo huo wa Tausi.
Alisema toka kuanza kwa mfumo huo mnamo mwezi Machi mwaka huu mafanikio yameanza kuonekana ikiwa ni pamoja na kuepusha upotevu wa mapato ya Halmashauri na wananchi kutopoteza muda kufuatilia huduma ikiwemo kulipa ushuru ama kuomba leseni ofisini kwakuwa mfumo huo unaruhusu kupata huduma popote walipo.
"Nature ya mfumo huu mtu mwenyewe anaweza kujisajiri kwa kuingiza taarifa zinazohitajika kwenye mfumo na hauhitaji kwenda kumsukuma mtu kila kitu anafanya huko alipo ikiwemo kupata control number na kulipia akiwa huko"aliongeza kusema Bw, Magambo.
Aidha aliwaomba wananchi kuhakikisha wao ndio wanajaza taarifa zinazohitajika na sio kumuagiza mtu kwakuwa katika usajiri itahitajika namba ya kitambulisho cha taifa (Nida),namba ya simu iliyosajiriwa kupitia Nida ambayo baadhi ya taarifa hutumwa kupitia namba hiyo.
"Changamoto inayojitokeza kupitia mfumo huu ni kuwa watu wengi hawana namba za Nida ama mwingine anakuwa namba ya Nida ila hana tena ile namba ya simu aliyoisajiri kwa Nida yake na mfumo unataka namba aliyosajiria Nida yake hivyo kujikuta walishindwa kumaliza kujaza taarifa zinazotakiwa ili kukamilisha maombi"alisema Ofisa hiyo.
Hata hivyo alifafanua kuwa katika kuhakikisha wananchi wa Monduli wanapata huduma hiyo tayari elimu kwa wadau na baadhi ya wataalam wa Halmashauri hiyo imetolewa ili kusaidia wananchi kujaza taafira kupitia mfumo huo ikiwemo watoa huduma za mtandao (internet services) katika maeneo ya Monduli mjini,Duka bovu,Lolkisale, Makuyuni,Mto wa mbu,Selela na Engaruka.
Naye mmoja wa wafanyabiashara ya saluni ya kike Bi,Stella Masanja akielezea mfumo huo alisema aliipongeza serikali kuanzisha mfumo huo na kusema unaongeza uaminifu kwa wananchi kwakuwa na uhakika wa mapato kuingia serikalini moja kwa moja.
Mfumo wa Tausi unamuwezesha mwananchi kuomba leseni,vibali na kulipa tozo,ushuru na faini mbalimbali kwa kutumia simu yenye uwezo wa kushika mtandao wa ama sehemu wanazotoa huduma za mtandao kupitia kompyuta huku lengo kuu la Serikali likiwa ni kuboresha ukusanyaji wa mapato Serikalini.



Wizara ya Maliasili na Utalii imemteua Rawan Dakik kuwa balozi wa hiari wa Mlima Kilimanjaro ikiwa ni kutambua jitihada zake za kutangaza Mlima Kilimanjaro nchini baada ya kupanda mlima Kilimanjaro kwa takriban mara tano na pia kuipeperusha bendera ya Tanzania katika kilele cha mlima mrefu zaidi duniani Everest uliopo bara la Asia.
Naibu Waziiri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo leo wakati wa hafla fupi ya mapokezi ya Rawan Dakik iliyofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro mkoani Kilimanjaro leo.
“Ni jambo la kujivunia sana leo hii kwa bendera yetu ya Tanzania kupeperushwa na si tu mwanamke wa kwanza kabisa Mtanzania lakini pia Mwanamke mwenye umri mdogo zaidi kufika kilele cha mlima Everest kutoka bara la Afrika”ameongeza Mhe. Masanja.
Mhe. Mary Masanja amesema kuwa Rawan Dakik amefanikiwa kufika katika kilele cha mlima Everest kutokana na jitihada binafsi alizojijengea baada ya kuanza kupanda Mlima Kilimanjaro tangu akiwa na umri wa miaka 13 kwa takriban mara tano.
”Mlima wetu wa Kilimanjaro umekuwa chachu ya mafanikio ya Rawan Dakik kwa kufika kilele cha mlima Everest kwa kuwa wataalam wanasema mlima Kilimanjaro ni moja ya kipimo muhimu cha kumuwezesha mtu kufanikiwa kupanda mlima Everest.” amesema Mhe. Mary Masanja.
Aidha, amesema mafanikio ya Rawan Dakik yatatoa hamasa kwa vijana wa Kitanzania hususan wasichana kutimiza ndoto zao.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Juma Raibu ameagiza kukamtwa kwa wazabuni wanane wanaodaiwa kula fedha za Halmashauri zaidi ya Sh47 milioni pamoja na viongozi wa vikundi 45 vya asasi za kuweka na kukopa (Vicoba).
Viongozi hao wanadaiwa kuwa wameshindwa kurejesha zaidi ya Sh94 milioni walizokopa tangu mwaka 2015.
Raibu ametoa agizo hilo alipowaita viongozi hao ofisini kwake kutaka kujua hatma ya fedha hizo ambazo walikopewa na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.
“Wote hapa niliowaita mmehujumu fedha za serikali, hili jambo linakera sana haiwezekani tangu mwaka 2015 mpaka leo hamjarejesha fedha hizi mnazodaiwa na Halmashauri zaidi ya Sh94 milioni, hili halikubaliki nawakabidhi leo mikononi mwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mtuambie mnarejeshaje fedha hizi,” Raibu
“Naomba muondoke na hawa watu watuambie tunapataje fedha zetu ambazo tuliwapa kwa upendo mkubwa, mimi sina mzaha kwenye fedha za serikali,” Raibu. “Takukuru naomba pia niwakabidhi wazabuni wanane waliokwapua fedha zetu za Halmashauri zaidi ya Sh47 milioni watuambie wanazirejesha hizi fedha za serikali,” Raibu
Na Imma Msumba, Mwanga
Wanawake wa Halmashauri ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro wametakiwa kutumia vizuri mikopo yao kwa kuwekeza kwenye shughuli mbalimbali za maendeleo na zitakazo zalisha kwa wingi na kuwaletea mapato yakutosha katika familia zao.
Ameyasema hayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mwanga Mhe.Saleh Mkwizu alipokutana na vikundi vya kina mama wajasiriamali wadogo wadogo waliojiajiri katika masoko na minada katika Kata mbalimbali za Halmashauri hiyo.
Mhe. Mkwizu amewataka wanawake hao kuonyesha kuwa wanaweza kuinuka kiuchumi na kuacha utegemezi huku wakitekeleza majukumu yao katika ngazi za familia na jamii kwa ujumla.
“Mikopo hiyo mnayoenda kupewa ichukulieni kama mmepata tunda la embe katika mti wa miba,mkaitumie vizuri mikopo hiyo na muache kwenda kununua vitu ambavyo havitawasaidia katika kujiletea maendeleo yenu na familia zenu"
Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu mpendwa mama Samia Suluhu Hassan imelenga katika kuhakikisha matunda ya nchi yanaliwa na kila mtanzania,hivyo fursa hiyo ya wanawake kupatiwa mitaji kwa mikopo isiyo na riba nimkakati mzuri wakuendelea kutelekeza Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Halmashauri yangu ipo tayari kuwasaidia wakimama wote watakao fanikiwa kumaliza marejesho yao na nitawasaidia kupata mikopo mingine ya riba nafuu huku mkiwa katika vikundi vyenu,pia muendelee kutafuta fursa kubwa zaidi katika miradi mikubwa inayofanywa na serikali,ili muweze kukua katika biashara zenu.
Pia nipende kuipongeza Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa juhudi wanazozifanya za kusaida makundi maalumu ya vijana,wanawake na wenye ulemevu katika Halmashauri ya Mwanga.
Niwasihi wadau wa maendeleo Wilaya ya Mwanga na wenye mapenzi mema kwa Halmashauri yetu waendelee kusaidia akinamama katika nyanja ya kujikwamua kiuchumi ile pale wanapokosa usaidizi basi waweze kusimama wao kama wao na kuendesha maisha yao na wategemezi wao.

.jpeg)



.jpeg)







