Naibu Waziri wa Uchukuzi Atupele Mwakibete akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, wakati Naibu Waziri huyo alipomtembelea Mkuu wa Mkoa huyo ofisini kwake hivi karibuni.
Imeelezwa kuwa upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Moshi mkoani
Kilimanjaro unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2023 ili kuruhusu ndege
zenye uwezo wakubeba abiria 40 za binafsi na za biashara kuweza kuruka na
kutua kiwanjani hapo.
Akizungumza mkoani humo mara baada ya kukagua maendeleo ya upanuzi
huo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amefafanua kuwa baada
ya filamu ya Royal Tour iliyofanywa na Rais wa Jamhuri wa Tanzania Mhe.
Samia Suluhu kumekuwa na ongezeko la watalii nchini hivyo dhamira ya
Serikali ni kuendeleza miundombinu ya viwanja vya ndege nchini ili
kutokwamisha matokeo ya filamu hiyo.
“Uzinduzi wa filamu ya royal tour umekuwa na matokeo chanya ambao
tunashuhudia idadi ya watalii inavyoongezeka kila siku, kwa ongezeko hilo
ndio maana mnaona tunajitahidi kuboresha viwanja vya ndege ili kuruhusu
watalii kuchagua popote wanapotaka kuruka na kutua," amefafanua Naibu
Waziri Mwakibete.
Aidha, Naibu Waziri huyo amezitaka Taasisi za Mamlaka ya Viwanja vya
Ndege nchini (TAA) na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS)
kuhakikisha wanamsimamia mkandarasi mzawa anayeboresha kiwanja hicho ili
akamilishe kazi hiyo kwa wakati na kwa viwango.
Mwakibete ameutaka uongozi wa TAA, TANROADS na Mkoa kukaa na
kumaliza changamoto zilizopo ikiwemo uvamizi wa eneo la kiwanja ili
kutomchelewesha mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Naye, Meneja wa TANROADS mkoa wa Kilimanjaro, Eng. Motta Kyando,
ameeleza kuwa upanuzi wa kiwanja hicho unagharimiwa na fedha za ndani
kiasi cha zaidi shilingi bilioni 12 na tayari Mkandarasi kampuni ya kizalendo ya
Rocktronic Limited ameanza kazi za awali za upanuzi ambapo mradi huo
utatekelezwa kwa muda wa miezi 12.
Eng. Motta ameongeza kuwa upanuzi huo utahusisha ujenzi wa barabara ya
kuruka na kutua ndege, barabara ya maegesho ya ndege, barabara za usalama
kiwanjani hapo kwa kiwango cha lami pamoja na uzio.
Kwa upande wake Meneja wa Kiwanja hicho, Yusufu Sood, amesema kwa sasa
kiwanja hicho kinahudumia ndege ndogo ambazo si za ratiba zinazoweza
kubeba abiria mpaka saba na helikopta za watu binafsi hivyo kukamilika kwa
maboresho hayo kutaongeza miruko ya ndege na idadi ya abiria.
Naibu Waziri Mwakibete yuko mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya siku mbili
ambapo anakagua miradi ya miundombinu ambayo inatekelezwa na Wizara
kupitia Taasisi za Sekta ya Uchukuzi.
Post A Comment: