Na Elizabeth Joseph, Monduli.


WANANCHI wilayani Monduli wameshauriwa kuhakikisha wanatumia Mfumo mpya wa ukusanyaji Mapato ya ndani ya Halmashauri (TAUSI) ili kuongeza ufanisi kwenye ukusanyaji wa mapato.

Ushauri huo umetolewa na Ofisa biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli Bw,Abdallah Magambo wakati wa mahojiano na chombo hiki kuhusu mfumo huo wa Tausi.

Alisema toka kuanza kwa mfumo huo mnamo mwezi Machi mwaka huu mafanikio yameanza kuonekana ikiwa ni pamoja na kuepusha upotevu wa mapato ya Halmashauri na wananchi kutopoteza muda kufuatilia huduma  ikiwemo kulipa ushuru ama kuomba leseni ofisini kwakuwa mfumo huo unaruhusu kupata huduma popote walipo.

"Nature ya mfumo huu mtu mwenyewe anaweza kujisajiri kwa kuingiza taarifa zinazohitajika kwenye mfumo na hauhitaji kwenda kumsukuma mtu kila kitu anafanya huko alipo ikiwemo kupata control number na kulipia akiwa huko"aliongeza kusema Bw, Magambo.

Aidha aliwaomba wananchi kuhakikisha wao ndio wanajaza taarifa zinazohitajika na sio kumuagiza mtu kwakuwa katika usajiri itahitajika namba ya kitambulisho cha taifa (Nida),namba ya simu iliyosajiriwa kupitia Nida ambayo baadhi ya taarifa hutumwa kupitia namba hiyo.

"Changamoto inayojitokeza kupitia mfumo huu ni kuwa watu wengi hawana namba za Nida ama mwingine anakuwa namba ya Nida ila hana tena ile namba ya simu aliyoisajiri kwa Nida yake na mfumo unataka namba aliyosajiria Nida yake hivyo kujikuta walishindwa kumaliza kujaza taarifa zinazotakiwa ili kukamilisha maombi"alisema Ofisa hiyo.

Hata hivyo alifafanua kuwa katika kuhakikisha wananchi wa Monduli wanapata huduma hiyo tayari elimu kwa wadau na baadhi ya wataalam wa Halmashauri hiyo imetolewa ili kusaidia wananchi kujaza taafira kupitia mfumo huo ikiwemo watoa huduma za mtandao (internet services) katika maeneo ya Monduli mjini,Duka bovu,Lolkisale, Makuyuni,Mto wa mbu,Selela na Engaruka.

Naye mmoja wa wafanyabiashara ya saluni ya kike Bi,Stella Masanja akielezea mfumo huo alisema aliipongeza serikali kuanzisha mfumo huo na kusema unaongeza uaminifu kwa wananchi kwakuwa na uhakika wa mapato kuingia serikalini moja kwa moja.

Mfumo wa Tausi unamuwezesha mwananchi kuomba leseni,vibali na kulipa tozo,ushuru na faini mbalimbali kwa kutumia simu yenye uwezo wa kushika mtandao wa ama sehemu wanazotoa huduma za mtandao kupitia kompyuta huku lengo kuu la Serikali likiwa ni kuboresha ukusanyaji wa mapato Serikalini.

Share To:

Post A Comment: