Wananchi wametakiwa kuwajali na kuachana na vitendo vya unyanyapaa dhidi ya wagonjwa wa kifafa, kwani asilimia kubwa ya wagonjwa hao hushindwa kupata ushirikiano kutoka kwa familia na jamii zinazowazunguka, jambo linalosababisha kuchelewa kupata matibabu na kufika hospitalini wakiwa katika hali mbaya zaidi kiafya.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kifafa Duniani yaliyofanyika leo Februari 06, 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) amesema kuwa wizara inaandaa miongozo na taratibu mbalimbali kuhakikisha kuwa wagonjwa wa kifafa wanaishi katika mazingira salama na yenye staha.

"Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kuwa watu takribani milioni 50 duniani wanaishi na kifafa, huku milioni 6 wakigundulika kila mwaka. Watu wenye kifafa wana hatari ya vifo mara tatu zaidi, huku Afrika ikiripoti viwango vya juu mara 4 hadi 6 zaidi. Zaidi ya asilimia 80 ya mzigo wa kifafa duniani unabebwa na nchi zenye kipato cha chini na cha kati, ikiwemo Tanzania.” amesema Dkt. Samizi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Dkt. Julieth Magandi, ameeleza kuwa Unyanyapaa bado ni changamoto kubwa kwa wagonjwa wa kifafa kwani baadhi ya jamii bado wanaamini kifafa kinarogwa, ni laana au ni ugonjwa wa kurithi, hali ambayo si ya kweli. Ameongeza kuwa kifafa ni ugonjwa unaotibika na kudhibitika kitaalamu, hivyo jamii inapaswa kuachana kabisa na mila potofu na badala yake kuwapa wagonjwa hawa msaada na heshima wanayostahili.

Aidha, akiwasilisha wasilisho lake katika mkutano huo, Rais wa Chama cha Kifafa nchini, Profesa William Matuja, amesema kuwa elimu kwa jamii ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya kifafa, akisisitiza kuwa endapo jamii itaelimishwa ipasavyo, wagonjwa wengi watajitokeza mapema kupata matibabu na kuishi maisha ya kawaida kama watu wengine.






Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: