Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa umeme kwenye vitongoji ni chachu ya kuinua uchumi wa wananchi vijijini.

Mhe. Sendiga ameyabainisha hayo leo Mkoani Manyara wakati wa kikao na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kilicholenga kumtambulisha Mkandarasi Mzawa aliyeshinda zabuni ya kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji 267 kwa mkoa huo, Kampuni ya SAGEM COM ENERGY.

Mradi huo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 45.8 unatarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu ambapo Vitongoji katika Wilaya za Babati, Hanang, Mbulu, Kiteto, na Simanjiro vitanufaika na mradi huo.

“Tunamshkuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo zinazowezesha kutekelezwa kwa mradi huu muhimu unaokwenda kuendelea kuinua uchumi wa maisha wa wananchi wetu hasa wa vijijini,” amesema Mhe. Sendiga.

Mkuu huyo wa Mkoa pia amewataka wakandarasi kufanya kazia kwa bidii na weledi na kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliopangwa huku akitoa rai kwa viongozi wa serikali pamoja na wananchi kutoka ushirikiano kwa mkandarasi wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

“Nikiwa kama Mkuu wa Mkoa natoa maelekezo kwa Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya kuhakikisha kuwa wanashirikiana na wanaenda kumtambulisha mkandarasi kwa wananchi. Lakini pia nitoe rai kwa wananchi, miradi hii ya kijamii ambayo inakwenda kutupatia faida kubwa tuipokee, tupunguze vikwazo,” amesisitiza Mhe. Sendiga.

Awali akizungumza kuhusu utekelezwaji wa mradi huo, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Herini Mhina amesema kuwa Mkoa wa Manyara unajumla ya Vitongoji 1946 na vitongoji 1113 tayari vimefikishiwa umeme.

Mhandisi Mhina ameongeza kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote nchini viwe vimefikishiwa nishati ya umeme na kwamba REA ikiwa na dhamana hiyo imejipanga kikamilifu kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati kufikia dhamira hiyo.

Share To:

Post A Comment: