Na Oscar Assenga, Lushoto
Kampuni ya Taifa Gesi imeendelea kujipambanua kama kinara wa usambazaji wa gesi nchini Tanzania, ikiwa na takribani asilimia 51 ya ujazo wa gesi yote inayopatikana nchini.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Meneja wa Masoko wa kampuni hiyo, Oscar Shelukindo, amesema kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya kuhifadhi na kusambaza gesi, pamoja na dhamira ya dhati ya kuwahudumia Watanzania.
Ameeleza kuwa lengo kuu la kampuni hiyo ni kusaidia juhudi za taifa za kuhamasisha matumizi ya nishati safi, kwa kuwahamasisha wananchi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, ambayo yamekuwa na athari kubwa kwa afya na mazingira.
Kwa mujibu wa takwimu, zaidi ya Watanzania 33,000 hufariki kila mwaka kutokana na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya nishati zisizo safi. Hali hiyo imeifanya Taifa Gesi kuongeza juhudi za kuhakikisha gesi inapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Katika hatua hiyo, kampuni hiyo inatoa mitungi ya gesi ya kilogramu 6 na 15 kwa bei nafuu, pamoja na huduma ya kujaza mitungi kwa wateja waliokwisha kuwa nayo, hatua inayolenga kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Aidha, Taifa Gesi kwa kushirikiana na NMB Bank wanatarajiwa kushiriki katika Tamasha la Kijiji Day, ambapo watatoa huduma mbalimbali pamoja na elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya nishati safi.
Juhudi hizi zinatajwa kuwa chachu ya mabadiliko chanya, zikilenga kuboresha afya za Watanzania na kulinda mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


.jpg)
.jpg)

Post A Comment: