Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amelieleza Bunge kuwa Marekani na Uingereza zilifunga Ofisi Ndogo za Ubalozi Zanzibar kutokana na mabadiliko ya kisera katika uendeshaji wa ofisi zao ndogo duniani kote na si kwa Tanzania pekee na kwa sasa yaliyokuwa majukumu ya ofii hizo yanaendeshwa na Ofisi za Balozi zilizoko Dar es Salaam.

Waziri Kombo amesema hayo alipojibu swali Bungeni Mei 25, 2026 jijini Dodoma ambapo aliongeza kuwa Serikali ya Italia ina Ofisi Ndogo ya Ubalozi iliyoko Kiembesamaki, Zanzibar na kwamba Serikali ya Italia imepandisha hadhi ofisi hiyo kutoka Konseli ndogo hadi Konseli Kuu na Bw. Stefano Totisco amethibitishwa kuwa Konseli Mkuu wa Italia hapa nchini.

Alisema kuwa hatua hiyo inaifanya Italia kuwa na uwakilishi mkubwa zaidi Zanzibar kwa ajili ya kushughulikia masuala ya wananchi wake pamoja na kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kijamii pamoja na Watanzania wenye uhusiano wa biashara, safari na uwekezaji na Italia utaimarishwa zaidi.

Waziri Kombo alisema Serikali inatambua umuhimu wa nchi rafiki kuwa na Ofisi Ndogo za Ubalozi Zanzibar kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa biashara, uwekezaji, utalii, siasa na utamaduni na kwamba ofisi hizo pia zina nafasi muhimu katika utoaji wa huduma za kikonseli kwa mujibu wa Mkataba wa Vienna wa mwaka 1963 unaosimamia uhusiano wa kikonseli duniani.

Akijibu swali la nyongeza, aliongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaendelea kuzungumzo na nchi mbalimbali ili kuzishawishi kufungua au kupandisha hadhi ofisi zao Zanzibar. Alitaja nchi hizo kuwa ni Uswisi, Ujerumani, Sweden, Norway na Brazil kwamba tayari nchi hizo zimeonesha dhamira ya kuimarisha uwakilishi wao Zanzibar.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: