Mbunge wa Jimbo la Hanang Mkoani Manyara ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Mhe. Asia Halamga, amekabidhi mifuko ya mbegu za dengu kwa viongozi na wananchi mbalimbali wilayani Hanang  ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha sekta ya kilimo na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza katika hafla ya ugawaji wa mbegu hizo Mbunge huyo amesema kuwa lengo la kutoa mbegu hizo ni kuongeza tija kwa wakulima na kuinua kipato chao kupitia kilimo cha kisasa hususani baada ya mvua nyingi za mwaka huu kuharibu mazao ya maharage shambani

Asia ameendelea kueleza kuwa  kuwa utoaji wa mbegu hizo utasaidia kurejesha uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula kwa wakazi wa Hanang kwani mbegu za dengu ni mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara yenye soko la uhakika ndani na nje ya nchi.

Kwa upande Mkuu wa Wilaya ya Hanang Almishi Issa Hazali amemshukuru Mbunge Asia Halamga kwa kuwakumbuka wananchi wa Jimbo hilo na kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi

“Hatua hii ni ya kupongezwa kwani inaenda moja kwa moja kugusa maisha ya wananchi wetu na sisi kama Serikali tutaendelea kushirikiana na Mbunge sambamba na viongozi wengine wote wenye nia njema ya kuleta maendeleo katika Jimbo letu hili,” Amesema Almishi

Hata hivyo wananchi hao wamemshukuru sana Mbunge huyo kwa msaada huo ambao utaleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo.




Share To:

Post A Comment: