Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu Miradi ya Maendeleo na Fursa za Vijana kwa Mwaka 2025/26, Jijini Dodoma.



Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imeendelea kuongoza katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Jangwa la Sahara, kwa kufanya zaidi ya upasuaji 3,000 wa tundu dogo kila mwaka.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Dkt. Peter Kisenge, amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika sekta ya afya, pamoja na kuimarika kwa rasilimali watu, vifaa tiba na miundombinu ya kisasa.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 9, 2026 jijini Dodoma, amesema Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyoanzishwa mwaka 2015 kwa ajili ya huduma za kibingwa bobezi, tafiti na mafunzo, imefanikiwa kupunguza utegemezi wa wagonjwa kwenda nje ya nchi kwa matibabu ya moyo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa ya moyo yanaongoza kwa kusababisha vifo duniani, yakigharimu maisha ya watu milioni 17.9 kila mwaka, huku asilimia 75 ya vifo hivyo vikitokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati.

Dkt. Kisenge amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika zilizoanzisha hospitali maalum za moyo kutokana na uwekezaji mkubwa unaohitajika.

Ameongeza kuwa JKCI hufanya zaidi ya upasuaji 3,000 wa tundu dogo kila mwaka pamoja na zaidi ya upasuaji mkubwa 800 wa kufungua kifua. Pia hutoa huduma za upasuaji tata kama TAVI, pamoja na upasuaji maalum kwa watoto ikiwemo Ozaki na Truncus.

Mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuwa kitovu cha utalii wa matibabu, huku wagonjwa kutoka ndani na nje ya Afrika wakija kupata huduma katika taasisi hiyo.

Katika kusogeza huduma karibu na wananchi, JKCI imeanzisha matawi sita katika maeneo ya Tazara (Temeke), Kawe, Oysterbay, Kariakoo, Chato na Arusha. Hali hii imeongeza idadi ya wagonjwa kutoka wastani wa 400 kwa siku mwaka 2022 hadi zaidi ya 1,100 mwaka 2025.

Aidha, taasisi hiyo imepanua huduma za upasuaji kwa watoto kupitia ufadhili wa Serikali na wadau, ambapo mamia ya watoto wamefanyiwa upasuaji bila malipo.

Kwa upande wa teknolojia, JKCI inatumia mifumo ya kisasa ikiwemo DOZEE kwa ufuatiliaji wa wagonjwa pamoja na mfumo wa miadi kwa njia ya mtandao uliopunguza msongamano na muda wa kusubiri huduma.

Taasisi hiyo pia imeanza maandalizi ya kuanzisha huduma za upandikizaji wa moyo, zikitarajiwa kuanza ifikapo mwaka 2030.

Zaidi, Serikali imewekeza katika maabara ya kisasa inayotumia teknolojia ya akili mnemba na roboti, hatua iliyopunguza muda wa majibu ya vipimo kutoka saa tatu hadi saa moja.

JKCI pia imeingia makubaliano ya ushirikiano na nchi mbalimbali za Afrika katika kuboresha huduma na kujenga uwezo wa wataalamu wa afya. Aidha, imeanzisha mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo (CardioTan) unaowakutanisha wataalamu kutoka zaidi ya nchi 40 duniani.

Kupitia huduma za tiba mkoba, taasisi hiyo imewafikia wananchi zaidi ya 35,000 katika mikoa mbalimbali nchini.

Katika mwaka 2025 pekee, JKCI ilitoa huduma kwa wagonjwa 252,915 huku wagonjwa 2,710 wakifanyiwa upasuaji, wakiwemo 836 waliopata upasuaji mkubwa wa moyo.
Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: