Dkt. Kiruswa aongoza ujumbe wa Tanzania katika kongamano la kikanda
Mbibo: Ushirikiano wa kimataifa ni chachu ya mafanikio Sekta ya Madini
📍 Addis Ababa, Ethiopia
Serikali ya Tanzania imesisitiza umuhimu wa matumizi endelevu ya madini muhimu (critical minerals) kama nyenzo kuu ya kuchochea maendeleo ya viwanda na kukuza uchumi Barani Afrika.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, Aprili 28, 2026, wakati wa kongamano la Kikanda lililofanyika Makao Makuu ya Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) jijini Addis Ababa.
Dkt. Kiruswa amesema Afrika ina nafasi ya kimkakati duniani kutokana na utajiri wa madini muhimu yanayotumika katika teknolojia za nishati safi, akitaja madini ya lithiamu, kobalti na nikeli kuwa nguzo muhimu katika uzalishaji wa betri za magari ya umeme na mifumo ya nishati jadidifu. Amesema hali hiyo inaifanya Afrika kuwa mhimili muhimu katika mabadiliko ya uchumi wa dunia kuelekea matumizi ya nishati safi.
Aidha, Dkt. Kiruswa ameongoza ujumbe wa Tanzania katika Kongamano hilo, ambapo ameeleza dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kuhakikisha rasilimali za madini zinasimamiwa kwa manufaa ya wananchi kupitia Sera na Mikakati inayolenga uongezaji thamani wa madini ndani ya nchi, ajira na ukuaji jumuishi wa uchumi.
Awali, Aprili 27, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo, alisema Afrika ina fursa kubwa ya kunufaika na ongezeko la mahitaji ya madini hayo duniani, lakini akasisitiza umuhimu wa kuhakikisha uwekezaji unaendana na misingi ya uendelevu na uwajibikaji.
Alibainisha changamoto zinazoikabili sekta ya madini kuwa ni pamoja na uchimbaji usio rasmi, uharibifu wa mazingira na ushirikishwaji mdogo wa jamii, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kukabiliana nazo.
Pamoja na Mambo mengine, Mbibo aliongeza kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa sambamba na kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za uchimbaji ili kuongeza tija na kupunguza athari kwa mazingira.
Kongamano hilo limewakutanisha mawaziri, wataalamu na wadau wa sekta ya madini kutoka nchi mbalimbali za Afrika na nje ya bara hilo, likilenga kujadili namna bora ya kuhakikisha madini muhimu yanachangia kikamilifu maendeleo ya viwanda na ustawi wa jamii.
Miongoni mwa washiriki mashuhuri ni Hailemariam Desalegn na Habtamu Tegegne, ambao kwa pamoja wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda ili Afrika inufaike ipasavyo na rasilimali zake za madini.

Post A Comment: