Na Saidina Msangi na Asia Singano, WF - Dodoma

Wizara ya Fedha imeendelea kutoa elimu kwa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata ufafanuzi kuhusu masuala ya kodi, uchumi na sera mbalimbali za fedha na mchango wa kodi katika kugharamia huduma muhimu za kijamii kama vile miundombinu, elimu, afya, maji nishati na huduma nyingine muhimu.

Hayo yamebainishwa na Afisa Usimamizi wa Fedha Mkuu, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. Abdul Dachi, wakati akitoa elimu kwa wananchi kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Bw. Dachi alisema kupitia Maonesho hayo, Idara imekuwa ikitoa taarifa kwa wananchi kwa lugha rahisi na inayoeleweka ili kuwawezesha kufahamu mchango wa Sera za Kodi na Uchumi katika maendeleo ya Taifa na ustawi wa jamii.

‘‘Miongoni mwa maeneo yanayotolewa elimu ni kuhusu mwenendo wa uchumi wa Taifa na namna Sera za Uchumi zinavyosaidia kudhibiti mfumuko wa bei, kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi kwa ujumla pamoja na namna hizo zinavyoandaliwa ili kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya Taifa,’’, alisema Bw. Dachi.

Aliongeza kuwa Serikali inatumia taarifa za takwimu na tafiti mbalimbali zinazosaidia katika upangaji wa bajeti na utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya muda mfupi na mrefu pamoja na usimamizi wa mikataba ya kikodi kati ya Tanzania na mataifa mengine na ushirikiano wa kikanda na kimataifa unaolenga kulinda maslahi ya Taifa katika sekta ya kodi.

Alifafanua kuwa wananchi wanapatiwa elimu kuhusu namna Wizara inavyofanya tafiti za kisera na kuandaa mapendekezo ya kitaalamu yanayosaidia Serikali kufanya maamuzi yenye tija kwa maendeleo ya nchi pamoja na namna Serikali inavyoshughulikia masuala ya kodi za kimataifa.

‘’Tumetumia fursa hii kueleza wananchi umuhimu wa sera za kodi na fedha katika kukuza uchumi na ustawi wa wananchi, mchango wa kodi katika maendeleo ya Taifa, pamoja na umuhimu wa uwazi na uwajibikaji katika mchakato wa utungaji wa sera nafasi ya Tanzania katika uchumi wa dunia na manufaa yanayotokana na ushirikiano wa kiuchumi na mataifa na taasisi mbalimbali za kimataifa’’, alifafanua Bw. Dachi.

Alisema kuwa ili kuhakikisha ujumbe unawafikia wananchi wengi zaidi, idara pia inatoa vipeperushi, vitabu vya elimu pamoja na mazungumzo ya ana kwa ana na wageni wanaotembelea Banda hatua inayochangia kuongeza uelewa wa umma na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wananchi katika maendeleo ya Taifa.

Share To:

Post A Comment: