Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linaendelea kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa yanayoendelea mkoani Dodoma, kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango na ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kutumika nchini.

Akizungumza katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TBS, Julius Lwenje, amesema kuwa shirika hilo lina jukumu la kusimamia na kuhakikisha bidhaa mbalimbali zinazozalishwa, kuingizwa na kuuzwa nchini zinakidhi viwango vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria.

Amesema TBS inaendelea kutoa huduma za ukaguzi, upimaji na uthibitishaji wa ubora wa bidhaa mbalimbali, ikiwemo vyakula na vinywaji, kwa lengo la kulinda afya, usalama na maslahi ya watumiaji.

Lwenje amewahimiza wananchi kuendelea kutumia bidhaa zenye alama ya ubora ya TBS, akieleza kuwa alama hiyo ni uthibitisho kwamba bidhaa husika imefanyiwa ukaguzi na imekidhi viwango vinavyotakiwa.

“Tunawaomba wananchi kuwa makini wanaponunua bidhaa na kuhakikisha wanachagua bidhaa zenye alama ya ubora ya TBS, kwani hii ni ishara kwamba bidhaa hizo zimehakikiwa na kuthibitishwa kuwa salama kwa matumizi,” amesema.

Aidha, amesema ushiriki wa TBS katika maadhimisho hayo unatoa fursa kwa wananchi kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na shirika hilo pamoja na kuelewa mchango wa viwango katika kukuza biashara, kulinda walaji na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanawakutanisha taasisi mbalimbali za Serikali na wadau wake kwa lengo la kuonesha huduma wanazotoa na kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na wananchi.





Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: