Na Oscar Assenga, Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Balozi Batilda Burian, amesema mkoa huo umeanza mkakati maalum wa kukuza na kutangaza utalii wa fukwe pamoja na fursa za uwekezaji zilizopo, ili kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.

Akizungumza leo, amesema ameita wadau mbalimbali kwa ajili ya kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuitangaza Tanga, akibainisha kuwa mkoa huo umejaliwa kuwa katika ukanda wa Bahari ya Hindi wenye maeneo mengi yenye fursa za kiuchumi na utalii.

Ametaja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni pamoja na Kipumbwi (Pangani), Ushongo, Kwale (Mkinga) na maeneo ya Raskazone jijini Tanga, ambapo kuna mradi wa kuboresha fukwe unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. 

Amesema mradi huo utakapokamilika utafungua fursa za michezo ya maji, matembezi ya boti, kuogelea pamoja na shughuli za kijamii kama harusi.

Aidha, amesema mkoa umeanza kushirikiana na Kampuni ya Makazi Solution pamoja na wadau wa Zanzibar ili kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuendeleza utalii wa fukwe.

 Timu ya wataalamu inatarajiwa kwenda Zanzibar kukutana na Wizara ya Utalii na wadau wengine ili kuimarisha ushirikiano huo.

“Tunajifunza kutoka Zanzibar, ambako maeneo kama Nungwi na Paje yalianza kidogo lakini sasa yamekua vituo vikubwa vya utalii. Sasa ni wakati wa Tanga kuchukua nafasi hiyo,” amesema.

Kwa upande wa uwekezaji, Dkt. Burian ameeleza kuwa mradi wa Kipumbwi Satellite City, unaotekelezwa kwa ushirikiano na Halmashauri ya Pangani na Makazi Solution, unalenga kutoa fursa kwa wananchi na wawekezaji kupata viwanja na kuendeleza eneo hilo.

Amesema eneo la Kipumbwi lina umuhimu mkubwa kimkakati, likiwa kilomita 3 kutoka bandari ya Kipumbwi, kilomita 80 kutoka Tanga, kilomita 60 kutoka Zanzibar kwa njia ya bahari, na kilomita 180 kutoka Dar es Salaam. Pia ujenzi wa barabara ya Tanga–Pangani–Saadani–Bagamoyo unatarajiwa kufungua zaidi ukanda huo wa pwani.

Mbali na fukwe, mkoa wa Tanga una vivutio vingi vya utalii ikiwemo Mapango ya Amboni, Hifadhi ya Taifa ya Saadani, Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, Milima ya Usambara (Lushoto), pamoja na urithi wa kihistoria kama makaburi ya vita ya kwanza ya dunia na Kisiwa cha Toten.

Ameongeza kuwa Tanga pia ni kitovu cha utamaduni wa Kiswahili, likiwa na historia ya muziki wa taarab, vyakula vya asili, pamoja na kuwa chimbuko la lugha ya Kiswahili, ambapo mwanazuoni mashuhuri Sheikh Shaban Robert alizaliwa katika eneo hilo.

Kwa sasa, amesema mkoa unapokea wageni kutoka ndani na nje ya nchi, hususan kutoka Kenya, Ujerumani, Uholanzi na Uswisi, wanaovutiwa na historia, mazingira asilia na utamaduni wa Tanga.

Dkt. Burian amesema jitihada hizo zinaunga mkono azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza Tanzania kupitia kampeni ya Royal Tour na kuongeza idadi ya watalii.

Kwa upande wa uchumi, amesema mkoa wa Tanga kwa sasa unachangia takribani shilingi trilioni 9.8 katika pato la taifa, na una mpango wa kuongeza mchango huo na kufikia nafasi ya pili kitaifa baada ya Dar es Salaam ifikapo mwaka 2028.

Amehitimisha kwa kusema kuwa Tanga ni eneo sahihi kwa uwekezaji na utalii, akiwakaribisha wawekezaji na watalii kutoka ndani na nje ya nchi kuja kutumia fursa zilizopo.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: