
Na, Mwandishi Wetu, Muleba – Kagera
KAIMU Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Bw. Salum Kimbau amesema maandalizi ya Mpango wa Afya Moja kwa mkoa wa Kagera utaunufaisha mkoa huo kwa kuzingatia malengo yake ya kuboresha uratibu na utekelezaji wa Dhana ya Afya ya Moja na kuendelea kutatua changamoto zilizopo na zenye mwingiliano kati ya binadamu, wanyama na mazingira
Amezungumza hayo wakati akifungua kikao kazi cha wataalamu wa masuala ya Afya Moja kutoka sekta mbalimbali zikiwemo za afya, mifugo, mazingira, wanyamapori na kilimo ambao wamekutana katika Halmashauri ya Wilaya ya Muleba mkoani Kagera kwa siku tano kuanzia tarehe 27 Aprili hadi 01 Mei, 2026 ili kuandaa Mpango huo utakaotumika kubaini rasilimali zitakazosaidia kutatua changamoto na vihatarishi vya afya ya binadamu, wanyama na mazingira.

Bw. Kimbau amesema kuwa, mkoa utanufaika kwa uwepo wa Mpango huo kwani utaongeza tija katika kutatua changamoto zinazokabili sekta hizo hususan katika kuendelea kutatua changamoto za mwingiliano wa magonjwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na binadamu kwenda kwa wanyama.
“Tunashukuru kuufikia mkoa wetu wa Kagera, tunajua kuwa asilimia 75 ya magonjwa yanatokana na mwingiliano ulipo kati ya wanyama na binadamu, hivyo kuandaliwa kwa mpango kutasaidia utekelezaji wa Dhana ya Afya Moja kwa kushirikiana pamoja, hivyo utatusaidia kutatua changamoto zilizopo na kuwa na jamii salama,” alisema Bw. Kimbau

Aliongezea kuwa ufanisi wa mpango huu unategemea ushirikishwaji wa sekta zote zinazohusika ili kuleta matokeo chanya.
Naye Mratibu wa Maafa kutoka Idara ya Menejimenti ya Maafa sehemu ya Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Bi. Valentina Sanga amesema kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Serikali la CIHEB Tanzania kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani imeratibu maandalizi ya uwepo wa mpango huo huku akisihi kuunganisha nguvu ya pamoja katika kuhakikisha utekelezaji wake unaleta matunda yanayotarajiwa.

Aidha, aliwasihi wataalamu wa Masuala ya Afya Moja kutumia fursa hiyo kuja na Mpango utakaoinufaisha Kagera, kwa kuzingatia ni miongoni mwa Mikoa inayokumbwa na majanga ya mlipuko mengine yakichangiwa na mwingiliano wa wanyama na binadamu.

“Dhana ya Afya Moja (One Health) inatoa fursa ya kutambua uhusiano wa karibu kati ya afya ya binadamu, wanyama, na mazingira. Inasisitizwa kuendelea kujifunza zaidi dhana hii ili kutatua changamoto zilizopo zikiwemo za milipuko ya magonjwa na kuweza kuyakabili endapo yanatokea katika maeneo yetu,” alisisitiza Bi. Valentina

Aliongezea kuwa, Mpango huo utasaidia kutatua changamoto za masuala ya kiafya zinazotokea katika Halmashauri za mkoa wa Kagera, kujiandaa na kukabili majanga hayo ili kuwa na jamii salama kwa maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la CIHEB Tanzania, Bw. Mark Lwakatare alisema mradi wa Usalama wa Afya Duniani utaendelea kushirikiana na mikoa husika katika kuimairisha utekelezaji wa dhana ya Afya Moja ili nchi iweze kukabiliana na vihatarishi vya majanga mbalimbali.

“Mradi huu unashirikiana na Serikali kuboresha na kuimarisha utekelezaji wa afua mbalimbali kupitia dhana ya Afya Moja nchini, hivyo mradi utaendelea kushirikiana katika kujiandaa na kukabili athari katika afya ya binadamu, manyama na mazingira,” alisisitiza Lwakatare.

Post A Comment: