Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 22,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonn-DODOMA
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kuimarisha uzalishaji wa sukari nchini ili kupunguza utegemezi wa kuagiza sukari kutoka nje ya nchi kupitia upanuzi wa viwanda vya sukari.
Akiwasilisha Mpango wa bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Kapinga amesema viwanda viwili vya Mkulazi Holding Company Limited na Kilombero Sugar Company Limited vimefanya upanuzi mkubwa wa uzalishaji utakaoongeza upatikanaji wa sukari nchini.
Amesema baada ya upanuzi huo, Kiwanda cha Kilombero kitaongeza uwezo wa kuzalisha sukari kutoka tani 123,000 hadi tani 226,000 kwa mwaka, huku majaribio ya uzalishaji yakiwa yamekamilika na uzalishaji rasmi unatarajiwa kuanza mwezi Juni, 2026.
Kapinga amesema kwa upande wa Kiwanda cha Mkulazi, kimeongeza mtambo mpya utakaowezesha uzalishaji wa sukari ya viwandani (industrial sugar) kwa ajili ya matumizi ya viwanda mbalimbali nchini.
Amesema majaribio ya mitambo hiyo tayari yamefanyika kwa mafanikio na kiwanda kimefanikiwa kuzalisha tani 256 za sukari ya viwandani.
“Upanuzi huu utawezesha kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, kupunguza uagizaji kutoka nje pamoja na kuchochea ukuaji wa sekta ya viwanda,” amesema Kapinga.
Aidha, amesema kukamilika kwa miradi hiyo kutazalisha ajira za moja kwa moja 8,500 pamoja na ajira zisizo za moja kwa moja 25,000, hatua ambayo itaongeza kipato kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi.

Post A Comment: