Wataalam wa Tasnia ya Maziwa nchini wameonya juu ya matumizi holela ya dawa kwa mifugo ambayo husababisha uwepo wa masalia ya dawa katika maziwa, hali inayoweza kuhatarisha afya za walaji na kuathiri ubora wa bidhaa za maziwa.
Onyo hilo limetolewa wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Tasnia ya Maziwa kuhusu magonjwa yanayoambukizwa kati ya wanyama na binadamu pamoja na usalama wa maziwa yanayofanyika katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) Mei 19, 2026.
Mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa kwa wadau wa mnyororo wa thamani wa maziwa kuhusu umuhimu wa kuzalisha maziwa salama, yenye ubora na yanayokidhi viwango vya afya kwa walaji, sambamba na kuimarisha udhibiti wa matumizi ya dawa kwa mifugo ili kuepusha madhara kwa binadamu.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Mbeya, Afisa Mifugo wa Mkoa, Bw. Adam Mhagama, alisema kuwa Tasnia ya maziwa ina mchango mkubwa katika afya, lishe na uchumi wa wananchi, hivyo ni muhimu kwa wadau wote kuzingatia usalama wa maziwa kuanzia shambani hadi kwa mlaji wa mwisho.
Alisisitiza kuwa elimu hiyo itasaidia kupunguza hatari ya magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na kuongeza imani ya walaji kwa bidhaa za maziwa zinazozalishwa nchini.
Kwa upande wake, Mkufunzi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Prof. Hezron Nonga, alisema matumizi holela ya dawa kwa mifugo yanaweza kusababisha uwepo wa masalia ya dawa katika maziwa, jambo linaloweza kuhatarisha afya ya walaji na kuathiri ubora wa bidhaa za maziwa.
Alifafanua kuwa kupitia mafunzo hayo, wadau wanaelimishwa juu ya matumizi sahihi ya dawa, muda wa kusubiri kabla ya kuuza maziwa baada ya matibabu ya mifugo pamoja na mbinu bora za usafi na uhifadhi wa maziwa.
Naye Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Prof. George Msalya, alisema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali na wadau kuhakikisha Tasnia ya Maziwa nchini inakuwa salama, yenye ushindani na inayochangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa taifa.
Aliongeza kuwa elimu kuhusu dhana ya Afya Moja (One Health) ni muhimu katika kuunganisha afya ya binadamu, mifugo na mazingira ili kukabiliana na changamoto za kiafya zinazoweza kuathiri jamii.
Prof. Msalya pia aliwataka wadau wa Tasnia ya Maziwa kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uzalishaji wa maziwa salama huku akihimiza matumizi ya teknolojia bora na ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali, wataalam na wafugaji katika kuimarisha Tasnia hiyo.
Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo, mmoja wa washiriki na mdau wa Tasnia ya Maziwa mkoani Mbeya alisema elimu waliyoipata itawasaidia wafugaji na wasambazaji wa maziwa kuelewa umuhimu wa kuzalisha na kusambaza maziwa salama, yenye ubora na yasiyo na masalia ya dawa.








Post A Comment: