SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limezindua huduma za Maabara ya Metrolojia katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za ugezi kwa haraka, kwa ufanisi na kwa gharama nafuu zaidi kwa wadau wa ukanda huo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBS katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika leo Mei 14, 2026 mkoani Mbeya, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa TBS, Julius Lwenje, amesema kusogezwa kwa huduma hizo katika ngazi ya kanda kutasaidia kuongeza uzingatiaji wa viwango pamoja na kupunguza gharama kwa wadau.

Amesema huduma hizo zitasaidia kuimarisha ushindani wa bidhaa za ndani sambamba na kulinda walaji na jamii kwa ujumla kupitia matumizi sahihi ya vipimo.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TBS Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga, amesema kanda hiyo inahudumia mikoa ya Mbeya, Songwe, Njombe na Rukwa huku huduma za metrolojia zikigusa pia mikoa ya Katavi, Ruvuma na Iringa.

Amesema ukanda huo ni muhimu kiuchumi kutokana na uwepo wa shughuli kubwa za viwanda, kilimo, biashara, afya pamoja na sekta ya ujenzi.

“Ukuaji wa sekta hizi umeongeza mahitaji ya huduma sahihi za vipimo, hususan vya kimaabara, ili kuhakikisha vinatumika kwa usahihi katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na utoaji huduma,” amesema Alananga.

Aidha, amesema kuanzishwa kwa huduma hizo katika ngazi ya kanda ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya TBS ya kusogeza huduma karibu na wananchi, tofauti na hapo awali ambapo huduma hizo zilikuwa zinapatikana Dar es Salaam pekee.

Nao wadau wa huduma za metrolojia wamepongeza hatua hiyo wakisema itasaidia kupunguza gharama za usafiri na muda wa kufuata huduma Dar es Salaam, jambo litakaloongeza ufanisi katika shughuli za uzalishaji na biashara katika ukanda huo.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: