Waziri wa Afya, Omary Mchenjgerwa amesema Serikali imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kuongeza huduma za matibabu, kinga na elimu kwa jamii, hatua iliyochangia kuongezeka kwa kliniki za kisukari na shinikizo la damu nchini.
Akizungumza leo Mei 11, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Mchenjgerwa amesema wizara imeendelea kuimarisha uratibu na utekelezaji wa afua za magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu pamoja na magonjwa sugu ya mfumo wa upumuaji.
Amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, Serikali imeanzisha kliniki mpya 130 za huduma za kisukari na shinikizo la damu, na kufanya idadi ya kliniki hizo kufikia 168 kutoka kliniki 38 zilizokuwepo katika kipindi kama hicho mwaka 2025.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kliniki hizo zimepatiwa dawa muhimu, vifaa tiba pamoja na mafunzo kwa watumishi wa afya ili kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma kwa wananchi wenye magonjwa yasiyoambukiza.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma za kinga na uchunguzi wa magonjwa hayo kupitia kampeni mbalimbali za afya ikiwemo upimaji wa magonjwa yasiyoambukiza katika maeneo ya kazi, utoaji wa elimu kwa jamii pamoja na matembezi ya Kitaifa yanayohamasisha wananchi kufanya mazoezi.
Mchenjgerwa ameongeza kuwa Wizara pia imeendelea kutumia vyombo mbalimbali vya habari kutoa elimu ya uhamasishaji kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, hatua inayolenga kupunguza ongezeko la wagonjwa na madhara yatokanayo na magonjwa hayo nchini.
.jpeg)
Post A Comment: