Na Hassan Kimweri, WAF - Dodoma
Sekta ya afya nchini imepata mafanikio makubwa katika kipindi cha awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yaliyoongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kupitia ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba, uoatikanaji wa dawa pamoja na huduma za kibingwa na za dharura nchini.
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hayo leo Mei 11, 2026 wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Spika wa Bunge Mhe. Mussa Azan Zungu.
"Eneo la vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka elfu 10,153 mwaka 2021/22 hadi elfu 13,683 kufikia Machi 2026, sawa na ongezeko la vituo 3,530, Zahanati zimeongezeka kutoka elfu 7,189 hadi elfu 8,706 huku hospitali zikiongezeka kutoka mia 404 hadi mia 475 mwaka 2026," amesema Waziri Mchengerwa
Aidha, Waziri Mchengerwa amesema Serikali imeongeza majengo mapya katika hospitali mbalimbali zikiwemo Hospitali ya Muhimbili, KCMC, BMH, Bugando, Mirembe, pamoja na Kibong'oto huku ikiwa imejenga hospitali mpya 10 za rufaa za mikoa, kukarabati hospitali kongwe 50, kukamilisha maboma 980 ya zahanati na kujenga vituo vya afya 390.
Amesema, katika huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, Serikali imeongeza wodi za watoto wachanga kutoka 80 hadi 438 pamoja na vituo vya upasuaji wa dharura kutoka 445 hadi 630 ambayo ni mafanikio yaliyochangia kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 mwaka 2016 hadi vifo 104 mwaka 2022 kwa kila vizazi hai 100,000.
"Katika huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa, Serikali imenunua na kusimika vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi bilioni 241.6 ambapo mashine za MRI zimeongezeka kutoka 7 hadi 13, CT Scan kutoka 12 hadi 45 pamoja na Digital X-ray kutoka 147 hadi 559," amesema Waziri Mchengerea
Kwa upande wa chanjo, amesema watoto waliopata chanjo ya Pentavalent dozi ya tatu wameongezeka kutoka watoto milioni 2,093,412 hadi milioni 3,186,979 huku kiwango cha chanjo kikiongezeka kutoka asilimia 93 hadi 96, juu ya lengo la kimataifa la asilimia 90.
"Upatikanaji wa dawa na bidhaa za afya umeimarika, Serikali imetoa Shilingi trilioni 1.4 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba, viwanda vipya 11 vya dawa na vifaa tiba vimeanzishwa huku 'Tanzania Pharmaceutical Industries kikifufuliwa kwa ajili ya uzalishaji wa dawa za VVU nchini," amesema Waziri Mchengerea
.jpeg)
Post A Comment: