NA EMMANUEL MBATILO

Serikali imeanza rasmi kutoa mafunzo ya urubani kupitia Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), hatua inayotajwa kuwa utekelezaji wa maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kuimarisha sekta ya usafiri wa anga nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 13, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Prof. Mbarawa amesema Serikali ilikuwa imeahidi katika hotuba ya bajeti ya mwaka 2025/2026 kuanza rasmi utoaji wa mafunzo ya urubani katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), na kwamba ahadi hiyo tayari imetekelezwa.

Amesema mafunzo hayo yalianza kutolewa rasmi mwezi Julai 2025 ambapo wanafunzi 22 walidahiliwa na wanaendelea na masomo yao ya urubani.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hiyo imewezesha kupunguza gharama ambazo wanafunzi walikuwa wakitumia kwenda kusoma masomo ya urubani nje ya nchi, huku ikiendelea kuongeza uwezo wa ndani katika sekta ya anga.

Aidha, amesema kuanza kwa mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendeleza sekta ya usafiri wa anga na kuongeza wataalamu wazawa wenye uwezo wa kuendesha na kusimamia huduma za anga nchini.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: