Na Mwandishi Wetu

 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo atamuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kongamano la 13 la Jukwaa la Miji Duniani (13th World Urban Forum) litakalofanyika Baku, Azerbaijan kuanzia tarehe 17-22 Mei 2026.

 

Kongamano hilo litakalofanyika katika Uwanja wa Olimpiki wa Baku kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Makazi Duniani (UN-Habitat), linabeba kaulimbiu isemayo: “Makazi kwa Dunia: Miji na Jamii Salama na Imara.”

 

Jukwaa hilo la Miji Duniani litazikutanisha nchi mbalimbali zikijadili na kuweka mikakati ya pamoja ya namna miji inavyoweza kuwa chachu ya kuchochea maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

 

Aidha, Kongamano hilo la siku sita litahusisha ushiriki wa viongozi katika ngazi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wataalamu mbalimbali watakaojadili changamoto za kimataifa za makazi pamoja na kukuza maendeleo endelevu ya miji.

 

Kupitia kongamano hilo la Miji Duniani kutakuwa na mawasilisho na mijadala kutoka kwa Mawaziri ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kutoa tamko  litakalotolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo.

 

Mawasilisho na mijada ya mawaziri katika kongamano hilo la Miji Duniani yatatoa fursa kwa Tanzania kujifunza kutoka nchi nyingine mbinu bora zinazoweza kuboresha utekelezaji wa sera mbalimbali za maendeleo pamoja na kutoa uzoefu wake.

 

Ujumbe wa Tanzania katika Kongamano hilo la Jukwaa la miji Duniani unahusisha pia Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Profesa Riziki Shemdoe,  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera pamoja na Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila.

Share To:

Post A Comment: