Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Mei 22,2026 bungeni Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WIZARA ya Viwanda na Biashara imeliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Shilingi bilioni 137.8 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara nchini.
Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 104.1 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, ambapo Shilingi bilioni 78.0 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi na Shilingi bilioni 26.0 kwa matumizi mengineyo ya uendeshaji.
Akiwasilisha bajeti hiyo Bungeni leo Mei 22, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Shilingi bilioni 33.6 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, huku fedha zote za maendeleo zikitokana na vyanzo vya ndani vya Serikali.
Amesema bajeti hiyo inalenga kuendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji, kuongeza uzalishaji wa viwanda vya ndani, kukuza biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Post A Comment: