Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mhe. Stephen Wasira ameipongeza Menejimenti ya Chuo hicho kwa Kujenga ofisi za Walimu na kumbi za Mihadhara kwa kutumia Makusanyo ya Mapato ya ndani, na hivyo kusaidia kupunguza changamoto ya Ofisi na Madarasa iliyokuwa inaikabili Taasisi hiyo.
Mhe. Wasira ameyasema hayo leo baada ya kuzindua jengo lenye ofisi zinazoweza kutumiwa na Walimu zaidi ya Sabini na kumbi mbili za Mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi Mia sita kwa mara moja kwa kila kumbi.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Prof. Haruni Mapesa amesema kuzinduliwa kwa ofisi na kumbi za Mihadhara kutasaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa vyumba vya kufundishia na ofisi ambazo zitatumiwa na Watumishi.
Mkuu huyo wa Taasisi amebanisha kuwa dhamira kuu ya ujenzi huo ni kuboresha ustawi na kutoa huduma bora kwa Wanafunzi na Wafanyakazi.
Ameongeza kuwa ujenzi huo utasaidia kuongeza mapato ndani ya Taasisi kwani chuo kitaongeza udahili wa Wanafunzi pamoja na kuendeleza mazingira bora, rafiki na safi kwa Ustawi wa jamii ya Chuo.
Mradi huo umegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni Moja na Milioni Sitini na Saba.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano na Masoko
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
21.05.2026

Post A Comment: