Mbunge wa Arusha Mjini Mhe. Mrisho Gambo ameeleza kuwa ndani ya miaka minne ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, miradi mbalimbali kwenye sekta ya elimu na afya imefanyika, suala ambalo limeondoa changamoto mbalimbali kwa wananchi wa Jiji la Arusha.

Akizungumza na Wananchi wa Jimbo hilo leo Mei 10, 2025 wakati wa Mkutano wake wa hadhara kwenye soko kuu Jijini Arusha, Gambo amewashukuru pia wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya CRDB kwa namna ambavyo ilisaidia katika ujenzi wa Madarasa mawili kwenye shule ya Sekondari Moshono Jijini Arusha.

Ameeleza pia kuhusu maboresho makubwa ya huduma za afya Jijini Arusha, ikiwemo ununuzi wa mashine za Xray na CT-Scan kwenye Hospitali ya Mount Meru Jijini Arusha, akieleza kwamba miaka minne iliyopita hakuna Hospitali ya Serikali iliyokuwa na mashine ya CT-Scan, wananchi wakilazimika kutumia gharama kubwa kupata vipimo hivyo kwenye Hospitali binafsi.

Amemshukuru Rais Samia pia kwa  kwa ujenzi wa Jengo jipya la Jengo la wagonjwa wa Nje kwenye Hospitali hiyo, ambapo Rais Samia kupitia Bunge la Tanzania waliridhia kutoa Bilioni tatu kwaajili ya ujenzi wa jengo hilo muhimu kwa huduma za matibabu.

" Watu wakati mwingine wanakuja wanaenda pale wanapiga picha, ooh nimefanya hivi na hivi, Haya mambo hayafanyiki bila bajeti na ili bajeti ipatikane lazima Mbunge asimamie imara kule Bungeni, mwambie jirani yako ukienda kupiga picha basi tambua na kazi ya Mbunge ya kutetea bajeti kule Bungeni." Amesema Mhe. Gambo.

Katika hatua nyingine Mbunge huyo ameeleza kwamba kwasasa kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Arusha, wameanza mkakati maalum wa kuhakikisha wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari katika Jiji hilo wanapangiwa shule za karibu, hatua ambayo inatokana na malalamiko ya Wazazi na walezi kulalamika watoto wao kusoma shule za mbali na hivyo kulazimika kugharamia nauli wakati zipo shule zilizo karibu na makazi yao.

Share To:

Post A Comment: