NAIBU Waziri wa Habari,Utamaduni,Michezo na Sanaa,Hamis Mwinyiijuma amempongeza Mbunge wa Jimbo la Longido Mkoani Arusha ambaye pia ni Naibu Waziri wa Madini,Dkt Steven Kiruswa kwa kutekeleza kwa vitendo sera ya michezo nchi kwa kuendeleza mchezo wa riadha katika jimbo hilo.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la michezo Nchini (BMT),Neema Msita kwa niaba ya Mwinyijuma baada ya kumalizika kwa mbio za riadha zijulikanavyo kwa jina la Kiruswa Funrun Marathon zilizofanyika katika uwanja wa Longido na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM),viongozi wa riadha Mkoa wa Arusha na wilaya ya Longido na kuhudhuriwa na watu zaidi ya 800.
Mwinyijuma alisema Mbunge Kiruswa anapaswa kupongezwa katika kutekeleza kwa vitendo sera ya kukuza mchezo wa riadha na kuamua kujitoa na kuwapa nafasi washindi wanne kwenda kusomea vyuo vya michezo nchini Kenya ili waweze kuumudu vema mchezo huo.
Alisema mchezo wa riadha ni mchezo muhimu sana na ni ajira kubwa sana na kwa kuliona hilo ndio maana Kiruswa ametoa motisha kwa washindi kwenda katika vyuo vya riadha nchini Kenya kwenda kujifunza zaidi mchezo huo ili waweze kuwa wawakilishi wazuri katika michezo ya Kimataifa.
''Serikali inahitaji kwa kiasi kikubwa watu wa aina ya Kiruswa kwani ni kiongozi mwenye moyo wa kujitoa katika kutekeleza sera ya michezo nchini hivyo serikali tunampa pongezi katika kufanikisha hilo''alisema Mwinyijuma
Naye Mbunge Kiruswa alisema dhumuni la yeye kuamua kuwapeleka washindi wanne nchini Kenya kusomea zaidi mchezo wa riadha ni kwa sababu nchi ya Kenya inafanya vizuri katika mchezo huo na sio aibu kwa sisi watanzania kwenda kuongeza ujuzi kwao.
Alisema Kiruswa Funrun Marathon ambayo hufanyika kila mwaka katika kipindi cha mwezi mei mbali ya kujenga afya na kutokomeza magonjwa nyemelezi pia mchezo huo umekuwa ikiwakusanya vijana wengi katika jimbo la Longido na nje na kuratibiwa na uongozi wa riadha Mkoa ili kupata washindi vijana na wenye sifa katika mchezo huo.
Naibu Waziri huyo amewashukuru wadau wote waliofanikisha mbio hizo na kusema kuwa moyo wao wa kujitolea ndio umefanikisha Kiruswa Funrun kufanikiwa kwa kiasi kikubwa mwaka huu na kuwaomba wasichoke pindi watakapofuatwa mwakani.
Naye Mbunge wa Geita Vijijini,Joseph Kasheku maarufu kwa jina la Msukuma aliwataka wana Longido kutomtupa Kiruswa kwani Kiruswa ni Lulu adimu katika jamii ya wafugaji wa kimasai na kusema kuwa ni mtu mpole na msikivu lakini ni mchapakazi aliyeaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Msukuma alisema amekuja mara zaidi ya tatu katika jimbo la Longido na mara ya kwanza alipokuja kumnadi kwa mara ya kwanza mwaka 2018 na baadae kuaminiwa na Rais kwa kuwa amesoma vizuri na mwenye uelewa wa hali ya juu hivyo wanapaswa kumfikiria kuongoza tena jimbo hilo wakati ukifika kwa kuwa serikali inahitaji sana wasomi wa aina ya Kiruswa.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Longido,Salumu Kally amesema wialya ya Longido pamoja na kuwa na jiografia ngumu ila wananchi wake wanapenda michezo na ndio maana Kiruswa amekuwa akifanya mara kwa mara mashidano ya riadha na soka lengo ni kutaka kuwapa ajira vijana.
Wakati huohuo katika mbio za km 21 wanaume ,Poul Matiko ameshika nafasi ya kwanza na kufanikiwa kujinyakuliwa zawadi ya shilingi 500,000,Livingston Lameck alishika nafasi ya pili na kupata shilingi 300,000,mshindi wa pili Ezekiel Mollel alipata shilingi 250,000 na upande wa wanawake mshindi wa kwanza kwa mbio hizo alikuwa Paticia Mabena alipata zawadi ya shilingi 500,000 na mshindi wa pili Stella Makula alipata shilingi 300,000.
Mbio za km 10 wanaume mshindi wa kwanza Lowassa Sabore alipata shilingi 250,000,nafasi ya pili ilichukuliwa na Baltazal Baltazal alipata shilingi 200,000 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Mbaraka Kanyongo aliyeambula shilingi 150,000 na upande wa wanawake mshindi wa kwanza alikuwa Sarafina Abel alipata shilingi 250,000 na nafasi ya pili alikwenda kwa yunes Yohana alipata shilingi 200,000 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Dorin Kamsika aliyepata shilingi 150,000.
Post A Comment: