Waziri wa Madini Anthony Mavunde amezindua mradi wa uchimbaji Madini ya dhahabu kwa vijana, wanawake na wenye ulemavu kwa kutoa leseni za uchimbaji mdogo wa madini ikiwa ni utekelezaji wa Programu ya Mining For a Brighter Tomorrow (MBT).
Amezindua mradi huo leo Mei 03, 2025 katika viwanja vya shule ya sekondari Ingwe vilivyopo katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime Mkoa wa Mara ambapo ametoa leseni 48 za uchimbaji mdogo wa madini kwa wanufaika zaidi ya 2000 vijana, wanawake na wenye nahitaji maalumu.
Akizungumza katika hafla hiyo amesema, Wizara ya Madini imekamilisha maandalizi ya Programu ya MBT ambayo itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2030 ambapo Programu hiyo ni ya kimageuzi katika Sekta ya Madini ambayo imeanzishwa kwa ajili ya kushughulikia changamoto na kuboresha fursa kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum ili kuongeza ushiriki wa makundi hayo katika mnyororo wa thamani wa madini.
"Naomba nichukue fursa hii kumpongeza Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye yeye alitupa maelekezo kuhakikisha vijana, wanawake na wenye mahitaji maalumu wanashiriki kikamilifu katika shughuli za madini.
Naupongeza Mgodi wa Barrick North Mara kwa kutoa Leseni kwa Vijiji 13 ambazo zitaendana na msaada wa kiufundi kwa Vijana zaidi ya 2000 watakanaonufaika na mradi huu.
Tukio hili litasaidia kuondoa mahusiano hasi kati ya mgodi wa North Mara na wananchi wanaozunguka mgodi huo ambao walionekana mara kadhaa kuvamia mgodi huo.
Mradi huu wa kihistoria na wa kwanza kufanyika nchini baina ya serikali,Mgodi na wananchi wanaozunguka mgodi,umevutia ushiriki mkubwa wa wadau kama Benki ya Dunia(WB) na Baraza la Dhahabu Duniani(WGC) ambao wameonesha dhamira ya kusaidia utekelezaji wake.”Alisema Mavunde
Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara Mhandisi Apolinary Lyambiko amesema utoaji wa Leseni hizo una lengo la kuimarisha uhusiano mwema na jamii inayozunguka mgodi.
Akitoa salamu zake,Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mh. Mwita Waitara ameipongeza serikali pamoja mgodi kwa mradi huu ambao utatoa ajira nyingi kwa vijana wa Tarime na kuiomba serikali isaidie upatikanaji wa mitaji wa kuendesha shughuli za madini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Mtambi amempongeza Waziri Mavunde kwa namna anavyo wasaidia wananchi wa Mara hususan katika eneo la Sekta ya Madini ambapo amesema juhudi za Waziri huyo zinaonekana kwa vitendo na kuomba vijana hao wajengewe uwezo ili waweze kuchimba kwa tija.
Sambamba na hayo, Kanali Mtambi amemuomba Waziri Mavunde kutoishia kwenye utoaji wa leseni pekee bali pia kuliangalia suala la msaada wa kiufundi pamoja na mitaji ili kuwawezesha wachimbaji hao kufanya kazi kwa tija.
Naye, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA), John Bina amempongeza Waziri Mavunde kwa kuzindua mradi huo na kuwataka vijana, wanawake na wenye mahitaji maalumu kufanya kazi kwa kushirikiana na kuepuka migogoro isiyo ya lazima.