Na John Mapepele -Moshi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa leo amekagua uharibifu wa  barabara ya Spencon- Fongagate- Mabogini- Chekereni hadi Kahe yenye urefu wa kilomita 31.25 na kuiagiza  Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuanza mara moja kujenga kwa kiwango cha lami. 

Akizungumza  kwa nyakati tofauti na wananchi wa Mabogini na  Kahe amesema Serikali inakwenda  kujenga kwa kiwango cha lami Ili ipitike katika kipindi chote cha mwaka ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Aidha, amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi kwenda  kupata huduma ya afya na elimu.

" Kukamilika kwa barabara hii  kutasaidia wananchi wetu kufikisha mazao yao sokoni kwa maana ya Moshi Mjini  na maeneo mbalimbali nchini  hivyo kukuza kilimo cha mazao ya mpunga, mahindi na miwa ambayo yameonyesha kusitawi vema kwenye eneo hili" . Amefafanua Mhe. Mchengerwa 

Amesema katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo utahusisha ujenzi wa mitaro  mikubwa kwa pande zote mbili, madaraja na kuweka  mawe na kifusi ambapo utaifanye ipitike katika misimu yote ya mwaka.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu  wa TARURA,  Mhandisi Victor Seiff  amesema mradi wa ujenzi wa barabara hiyo hadi kukamilika kutagharimu takribani bilioni 45 ambapo awamu ya kwanza itagharimu jumla ya shilingi bilioni 7.

Pia Waziri Mchengerwa amezielekeza  Halmashauri zote nchini kukusanya mapato ya ndani na kuanza kutenga  10% kwa ajili ya ujenzi wa barabara.

Wakati huohuo amewaagiza wakuu wote wa mikoa na Wilaya kuendelea kulinda amani na kudhibiti vitendo vyovyote vinavyoweza  kusababisha uvunjifu wa amani.






Share To:

Post A Comment: