✅️ _Akemea Jasi Kuuzwa na Kununuliwa Chini ya Bei Elekezi_

✅️ _Aingilia Kati Kero kwa Wachimbaji Wadogo, Wadau Kukutana Dodoma Kutafuta Suluhu ya Kudumu_

✅️ _Awahimiza Vijana Kuchangamkia Fursa Zilizopo Sekta ya Madini_ 

✅️ _Mining For A Brighter Tomorrow-MBT Kimbilio Jipya kwa Vijana na Wanawake_

Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini inatarajia kukutana jijini Dodoma katika siku za karibuni na wadau wa madini ya jasi (gypsum) wakiwemo wachimbaji wadogo, wasafirishaji, wamiliki wa viwanda vya saruji, Uongozi wa Wilaya na Halmashauri ya Wilaya ya Same ili kujadili na kutatua changamoto zinazoathiri shughuli za uchimbaji na biashara ya madini hayo ambazo zimechangia kusuasua kwa maendeleo ya wananchi wanaotegemea sekta hiyo.

Alitoa kauli hiyo jana, Desemba 12, 2025, wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji katika Kata za Makanye na Ruvu Jeungeni, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro, ambako pia alizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya jasi.

Dkt. Kiruswa alisisitiza marufuku ya kununua madini ya jasi chini ya bei elekezi iliyotolewa na Tume ya Madini, akiwataka wote kuheshimu miongozo hiyo ili kulinda maslahi ya wachimbaji.

Kwa upande wa mazingira, alitoa wito kwa wachimbaji kuhakikisha utunzaji wa mazingira, kufukia mashimo mara baada ya shughuli za uchimbaji kukamilika, pamoja na kupongeza juhudi za uanzishwaji wa Mfuko Maalum wa kusaidia kurejesha mazingira mara baada ya kutamatika kwa shughuli za uchimbaji, ambao umeelezwa kuwa chachu ya kuimarisha uwajibikaji na uendelevu wa shughuli za madini wilayani humo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa aliendelea kusisitiza umuhimu wa mafunzo ya MBT kwa vijana na wanawake, utoaji wa leseni, pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kisasa ili kuongeza ufanisi na usalama katika uchimbaji mdogo wa madini ya jasi na kuwahimiza vijana kuchangamkia fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa Sekta ya Madini. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni alieleza kuwa uchimbaji wa jasi ni uti wa mgongo wa maendeleo ya wananchi na Halmashauri ya Wilaya ya Same, na kwamba kuibuka kwa mgogoro huo baina ya wachimbaji wadogo na wamiliki wa viwanda vya saruji unakwamisga maendeleo katika wilaya hiyo na kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na tija kwa wadau wote.

Naye, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Abel Madaha alisema kuwa Tume ya Madini kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali pamoja na wadau wa madini wamekuwa wakikaa mara kwa mara kwa manufaa ya wachimbaji na watumiaji wa madini husika ikiwemo kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakumbuka wachimbaji kuanzia migodini hadi kwa watumiaji wa mwisho.











Share To:

Post A Comment: