Na Mwandishi Wetu,DODOMA

MBUNGE wa Viti Maalumu Kupitia Kundi la Asasi za Kiraia Tanzania (NGOs) Neema Lugangira amesema kwamba akili mnemba (artificial intelligence - AI) ina tija na fursa nyingi katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya,Kilimo na Elimu na nyenginezo hapa nchini.

Aliyasema hayo wakati akizungumza katika Semina ya Akili Mnemba kwa Wabunge Wanawake iliyoandaliwa kwa Ushirikiano na Shirika ambalo alilianzisha la Omuka Hub pamoja na Bunge la Tanzania kupitia Mradi wa Female Al Leaders chini ya Women Political Leaders (WPL) na GIZ unaolenga kuimarisha Utawala Bora wa Akili Mnemba “Artificial Intelligence #Al” kwa kuimarisha Wanawake Wanasiasa barani Afrika ili waweze kuibeba ajenda hiyo na kuwa Vinara.

Alisema katika Semina hiyo wamejadiliana mambo mengi na imeonyesha akili mnemba inafursa nyingi lakini alitoa angalizo pia isipotumika kwa usahihi ina changamoto ikiwemo ukatili wa kijinsia, kurubuni watoto na inaweza kupelekea kufifisha uwezo wa kufikiria kutokana na kutufanya sisi kuwa tegemezi sana.

“Katika semina hii, akili mnemba imetushangaza sisi kama Wabunge sababu niliamua kufanya jaribio la kuiuliza hii AI swali kuwa mimi ni Mbunge na naelekea kwenye uchaguzi, naomba inisaidie kuniandalia mkakati wa kampeni na baada ya dakika chache AI ikanipa mkakati kabambe kwa usahihi hadi mwenyewe unashangaa na inakuwa na uwezo wa muda mfupi wa kupima kila kilicho kwenye mitaandao yote yenye uwezo nayo inakupa picha pana”, Alisema Mbunge Neema Lugangira.

Alisema kwamba Akili Mnemba ni kitu ambacho kina tija lakini tija hiyo ili iweze kupatikana lazima itumike kwa ufasaha na wao kama Wabunge ni kitu ambacho wanakwenda kukiangazia; ni lazima kama Tanzania iwepo sera ya akili mnemba pamoja na sheria ili kama taifa linufaike na faida zake na pia kujikinga na kudhibiti na madhara yanayoweza kupatikana kwenye eneo hilo la akila memba.

Awali akizungumza Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini (CCM) Jesca Msambatavangu alisema niwaondolee hofu akili mnemba haijaja kupora ajira za watu  bali imekuja kuboresha ajira na  kukuanzisha ajira na haijaja kumbagua mtu yoyote lakini lazima tutambue dunia ina mambo mazuri na mabaya hayo mambo wanatakiwa kujifunza mambo muhimu hivyo tunashukuru kuletewe semina hii ambavyo tunaamini itakuwa na tija”.

Naye kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii Fatma Toufiq alisema Bunge linatambua fursa na changamoto za akili mnemba hivyo Bunge wanajipanga kuandaa Sheria za Usimamizi.

Mbunge Fatma ambaye alimwakilisha Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson kwenye Semina hiyo ya Wabunge Wanawake kuhusu Akili Mnemba “Artificial Intelligence” ambapo alisema kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limefurahi kuwa sehemu ya kunufaika na mafunzo ya teknolojia ya akili mnemba.

Mhe Neema Lugangira (MB) ni mwakilishi Afrika wa Women Political Leaders (WPL)amefanikiwa kufanikisha mradi wa Female Al Leaders kuja hapa Tanzania ambapo sehemu ya kwanza ilikuwa ni kuandaa Semina ya Wabunge Wanawake kwa kushirikiana na Shirika ambalo alilianzisha la Omuka Hub pamoja na Bunge la Tanzania.


MWISHO.

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: