Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amefanya ziara katika Mgodi wa Williamson Diamond Limited uliopo Wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu malalamiko ya ulipaji fidia kwa wananchi walioathiriwa kutokana na kupasuka kwa bwawa la maji tope lililotokea Novemba, 2022.
Utekelezaji huo unafuatia ziara ya Kamati hiyo iliyoifanya tarehe 19 Februari, 2024 mgodini hapo ambapo iliitaka Serikali kufanya tathmini ya eneo lililopata madhara. Aidha, wakati wa ziara hiyo, kamati ilipata fursa ya kutembelea bwawa jipya lililojengwa pamoja na nyumba walizojengewa walioathiriwa na tope hilo.
Akizungumza katika ziara hiyo, Dkt. Kiruswa ameupongeza mgodi huo na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Shinyanga kwa kuendelea kutekeleza maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na kuwataka kuendelea kuzifanyia kazi kasoro zilizoonekana ili kuondoa manung’uniko machache yaliyopo kuhusu malipo ya fidia.
Vilevile, Naibu Waziri ameupongeza mgodi wa WDL kwa utekelezaji wa Kanuni kuhusu Wajibu wa Kampuni kwa Jamii ( CSR) na Local Content na kuutaka kutumia kiasi cha fedha za CSR kutoa elimu na ujuzi kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Williamson Mhandisi Ayoub Mwenda akieleza hatua za utekelezaji wa maelekezo ya kamati ya Bunge, amesema kupitia kamati ya kushughulikia migogoro inayojumuisha wenyeviti wa vijiji, madiniwani na mwakilishi kutoka Ofisi ya halmashauri ya Kishapo wameendeleea kukutana na waathirika kwa lengo la kuwasikiliza na kutatua malalamiko yao.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kishapo Mhe. Joseph Mkude, amesema kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa imeendelea kushughulikia malamiko yaliyopo na baada ya maelekezo ya Kamati ya Bunge imeenda katika eneo la walalamikaji kwa lengo la kuwasiliza na imeandaa taarifa.
Katika ziara hiyo Mhe. Naibu Waziri aliyoifanya leo Machi 20, 2024 ya kufuatilia utekelezaji wa maelekezo hayo ameongozana na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Mhe. Joseph Mkude ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Shinyanga na Afisa Madini Mkazi Shinyanga Bw. Daniel Mapunda.
Post A Comment: