Na Angela Msimbira, Dar es Salaam


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe Angellah Kairuki amewaomba wadau wa maendeleo nchini kushiriki katika kuchangia maendeleo ya elimu kwa kutoa kiasi cha fedha kitakachoiwezesha  Serikali kukidhi kigezo cha kupata ufadhili wa zaidi ya dola za Marekani milioni 50 kupitia Multplier Grant 2023. 

Mhe. Kairuki ametoa ombi hilo kwa wadau  wa elimu Mkoa wa Dar es Salaam Agosti 14, 2023  katika Ukumbi wa Anatouglo Jijini Dar es Salaam kwenye kikao kazi kilicholenga kuwajengea uelewa kuhusu dhana  ya GPE LANES  MULTIPLIER GRANT na kuwashawishi kuchangia maendeleo ya elimumsingi.

Mhe. Kairuki amesema endapo Tanzania itaweza kupata ufadhili huo fedha zake zitachangia katika kuiwezesha Serikali kutekeleza mipango mipya endelevu iliyoibuliwa na mabadiliko ya Sera na Mitaala ya Elimu hususani katika kufanikisha utekelezaji wa eneo la Mafunzo ya Amali.

Amesema kuwa kupitia ufadhili wa GPE Multiplier nchi 18 zimetengewa dola za Marekani milioni 50 kiwango cha juu cha mgao ‘Maximum Allocation’ kwa Mwaka 2023 ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo lakini fedha hizo zitatolewa kama nchi itakidhi kigezo cha wadau elimu nchini kuchangia.

Mhe. Kairuki amesema upatikanaji wa motisha hiyo unafuata hatua mbalimbali ambapo kila dola moja ya Marekani itakayotolewa kupitia sekta binafsi ikiwemo kampuni, asasi za kiraia na benki, Mfuko wa GPE utatoa dola moja ya Marekani.

Amesema kuwa kila dola tatu za Marekani zitakazotolewa kama msaada au msamaha wa fedha za mkopo kutoka katika taasisi za fedha za kimataifa au nchi washirika wa maendeleo, Mfuko wa GPE utatoa dola moja ya Marekani hivyo amewaomba wadau wa maendeleo ya elimu nchini kuchangia fedha.

“GPE wameonesha nia ya kutufadhili kiasi cha dola za Marekani milioni 50 baada ya wadau wa ndani kuonyesha nia ya kuchangia katika masuala ya elimumsingi, ninawaomba sana wadau wetu kuiwezesha nchi kupata fedha hiyo itakayotumika kuboresha miundombinu ikizingatiwa kuwa bado kuna uhitaji mkubwa, ” Mhe. Kairuki amesisitiza. 

Aidha, Mhe. Kairuki amesema kuwa ili kuweza kupata fedha kupitia ufadhili wa GPE Multiplier, wadau watatakiwa kuandika barua za kuweka nia ya kuchangia katika masuala ya elimumsingi ili kuwezesha nchi kujaza tamko la nia za wadau kuchangia kupitia Fomu ya “Expression of Interest (EoI) itakayotumika kama kigezo cha upatikanaji wa ufadhili huo.

Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: