Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kushirkiana na Uongozi wa Wilaya ya Karatu wamefanya kikao cha ujirani mwema kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kupunguza na kumaliza migogoro kati ya wananchi na Wanyamapori hatarishi kwa vijiji vya Wilaya ya Karatu vinavyozunguka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Akiongoza kikao hicho kilichohusisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Karatu Mhe. Dadi Kolimba ameeleza kuwa wamekubaliana na uongozi wa NCAA kuweka mikakati wa kupambana na wanyamapori hatarishi wanaongia kwenye mashamba na makazi ya watu.

Mhe. Kolimba amesema mikakati hiyo ni pamoja na kujenga uzio wa umeme wa kuzuia wanyama wanaoingia kwenye makazi na mashamba ya wananchi, kutengeneza mizinga ya Nyuki kudhibiti wanyama wakali kama tembo na kutoa elimu kwa jamii ya vijiji vyote vinavyozunguka Hifadhi ya Ngorongoro kujua namna bora ya kujilinda na wanyama wanaovamia maeneo yao.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Karatu Bw. Juma Hokororo ameeleza kuwa Halmashauri ya Karatu imejipanga kutoa vifaa kwa ajili ya askari na wataalam wa Wanyamapori wa wilaya hiyo kushirikiana na askari wa Uhifadhi wa NCAA ili kuelemisha wananchi namna ya kuchukua tahadhari, mbinu sahihi za kufukuza wanyama na kujiokoa pindi wanyama hatarishi wanapoingia katika jamii wanazoishi.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA Elibariki Bajuta amesema kufanyika kwa kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kukutana na uongozi wa maeneo yanayozunguka hifadhi na kwa pamoja kushirikiana katika kuweka mikakati ya kudhibiti changamoto zinazotokana na wanyamapori waharibifu.

Ameongeza kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika kupunguza migogoro ya Wananchi na wanyamapori kwa sasa imejipanga kujenga uzio wa umeme wenye urefu wa kilomita 30 kutoka lango kuu la Loduare kuelekea maeneo yenye muingiliano mkubwa wa wananchi na wanyamapori pembezoni mwa hifadhi ya Ngorongoro.

Naibu Kamishna Bajuta amesisitiza kuwa ushirikiano baina ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na jamii inayozunguka Hifadhi ni muhimu katika kupata utatuzi wa migogoro hiyo.

Ikumbukwe kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa Uhifadhi katika kubuni na kutatua changamoto zinazotokana na wanyamapori waharibifu katika maeneo yanayoizunguka Hifadhi.

Share To:

Post A Comment: