Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mjini Mhe. Benno Malisa akifungua mafunzo kwa Viongozi wa Umma kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Jengo la NHIF leo Mei 5,2023 Jijini Mbeya.

Katibu Msaidizi Kanda ya Nyanda za juu kusini -Mbeya Bw. Pauline Kanoni akitoa neno la ufunguzi katika hafla ya mafunzo kwa Viongozi wa Umma kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Jengo la NHIF leo Mei 5,2023 Jijini Mbeya.

Afisa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Nyanda za juu kusini- Mbeya Bw.Limuli Kibona akitoa mada kuhusu Maadili ya Viongozi wa Umma na Tamko la Rasilimali na Madeni katika mafunzo ya Viongozi kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya yaliyofanyika katika ukumbi wa jingo la NHIF leo Mei 5,2023 Jijini Mbeya.

Afisa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Makao Makuu Dodoma Bw, Evarist Msakila akitoa mada kuhusu Hati ya Ahadi ya Uadilifu katika mafunzo ya Viongozi kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya yaliyofanyika katika ukumbi wa jingo la NHIF leo Mei 5,2023 Jijini Mbeya.


Na.Mwandishi Wetu-MBEYA


MKUU wa Wilaya ya Mbeya Mjini Mhe. Benno Malisa,amewataka Viongozi wa Umma kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuweza katika kutekelezaji majukumu yao ya kila siku.


Hayo ameyasema wakati akifungua mafunzo kwa Viongozi wa Umma wa Halmashauri mbili za Mkoa wa Mbeya ambazo ni halmashauri ya Jiji la Mbeya na halmashauri ya Mbeya DC yaliyoandaliwa na Sekretariti ya Maadili ya Viongozi wa Umma yalifanyika katika Ukumbi wa Jengo la NHIF Jijini Mbeya.


 Mhe. Malisa alieleza kuwa ni dhahiri kuwa Viongozi wote katika Halmashauri hizo wanapaswa kufanya kazi kwa kushirikiana kwa pamoja , kuwa na mawazo na uelekeo mmoja ili kurahisisha utekelezaji wa shughuli zote za serikali na kuweza kuleta matokeo chanya kwa wananchi na serikali kwa ujumla.


Mhe. Malisa alifafanua kuwa serikali inapeleka fedha nyingi sana katika halmashauri mbalimbali nchini kwa sababu ndipo kunakotekelezwa miradi mingi inayowagusa wananchi moja kwa moja kama vile maji, elimu , afya na nyingine nyingi


“Ndugu zangu fursa hii tukaitumie vizuri ili matokeo ya fedha hizi yakaonekane wazi huu sio muda wa kulumbana, sio muda wa kususiana majukumu,sio muda wa kunyoosheana vidole bali ni muda wa kuunda timu moja , ni muda wa kila mmoja kuwajibika ipasavyo katika nafasi aliyo nayo na kufanya kazi kwa bidii ili tukaaminike kwa viongozi wetu wa juu ” alisema.


Aidha Mhe. Malisa aliendelea kusema kuwa Viongozi wanapowajibika kwa pamoja itarahisha utendaji kazi wao wa kila siku wa kuhakikisha kuwa wananchi wanatekelezewa miradi yote kama ilivyopangwa jambo linakalowafanya wananchi kuwa na Imani na viongozi wao na kuiamini serikali kwa ujumla wake “Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu” alisema.


Pamoja na hayo Mhe. Malisa alizungumzia suala la mgongano wa maslahi kuwa limekua ni tatizo kubwa sana katika Halmashauri nyingi nchini. Suala hili limekua na changamoto nyingi katika kutekeleza miradi mbalimbali, Kiongozi anapokua na maslah binafsi katika mradi fulani husababisha kucheleweshwa kwa miradi hiyo ama kutekelezwa kwa kiwango kisichoridhisha ama kutokutekeleza kabisa kutokana na mvutano unaokuepo baina ya watekelezaji kwa sababu ya maslah binafsi.” Viongozi wenzangu hatukuteuliwa tukafanye kazi kwa kuangalia maslah yetu binafsi, tumeteuliwa tukawatumikie wananchi bila kutanguliza maslah yetu mbele tukatangulize maslah ya wananchi na Taifa kwa ujumla: alisema.


Awali akielezea dhumuni kubwa la mafunzo hayo Katibu Msaidizi Kanda ya Nyanda za Juu kusini -Mbeya Bw, Pauline Kanoni alisema kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ina jukumu kubwa la kutoa elimu ya maadili kwa Viongozi wa Umma nchini ili kuwa na Viongozi waadilifu na wenye kuaminika kwa wanachi wao.


Pamoja na hayo Bw. Kanoni alisema kuwa mafunzo hayo yana lengo la kuwakumbusha Viongozi kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Namba 13 ya mwaka 1995. Katika kuzingatia sheria hii yapo mambo ambayo viongozi wanapaswa kuzingatia wanapotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia kanuni za Maadili pamoja na misingi ambayo imewekwa kulingana na sheria na katiba , kuwa wawazi kwenye shughuli wanazofanya na kutumia rasilimali za Umma vizuri.


” Niwaase Viongozi kuwa na uwajibikaji wa pamoja katika kutekeleza majukumu yenu kwani haiwezekani Kiongozi anakwenda kinyume na maelekezo ya serikali , unakuta kingozi huyu anasema hivi mwingine anasema hivi hayo sio maadili viongozi wote wanapaswa kuwa na kauli moja“ alisema.


“Tunajua viongozi wetu sio kwamba hamna Maadili tunajua kuwa ni waadilifu wa kutosha lakini tumekuja kukumbushana tuu kwa sababu tunajua binadamu tunasahau hivyo tunakumbushana nini tunapaswa kufanya nini hatupaswi kufanya wakati wa utekelezaji wa majukumu yetu kwani kiongozi akikiuka maadili anaitia doa serikali yetu” alisema


Naye mshiriki wa mafunzo hayo Afisa Kilimo katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya Bi. Amina Nalicho alisema kuwa ili kuweza kupata matokeo chanya kwa serikali na wanachi ni dhahiri kuwa Viongozi wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja “ kuna msemo usemao kidole kimoja hakivunji chawa” alisema.


Katika mafunzo hayo ya siku moja yalitolewa kwa viongozi wapya ambao ni wakuu wa idara na vitengo kutoka Halmashauri ya Mbeya Jiji pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya . Mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwa ni pamoja na Mada ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Tamko la Rasilimali na madeni, mada ya Ahadi ya Uadilifu,Mada ya Mgongano wa maslah Pamoja na mada ya uwajibikaji wa Pamoja.

Share To:

OKULY BLOG

Post A Comment: