KatibuTawala  Mkoa wa Singida, Dk.Fatma Mganga akifungua mkutano wa wadau wa Bohari ya Dawa (MSD) uliofanyika Mei 3, 2023 mjini Singida. Kulia ni Meneja wa MSD Kanda ya Kati, John Sipendi na kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Victorina Ludovick. 

Na Dotto Mwaibale, Singida 

BOHARI ya Dawa (MSD) imefanya maboresho katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuingia mikataba ya muda mrefu na wazalishaji ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za afya nchini. 

Hayo yamesemwa na Meneja wa MSD Kanda ya Kati, John Sipendi wakati akimkaribisha mgeni rasmi KatibuTawala wa Mkoa wa Singida, Dk.Fatma Mganga kufungua mkutano wa wadau wa MSD uliofanyika mjini hapa hivi karibuni na kuhudhuriwa na Mganga Mkuu wa mkoa, Waganga Wakuu wa Wilaya,Wafamasia,Wataalam wa maabara na viongozi wa MSD.

Sipendi alisema ili kufikia dira na kutimiza dhima na malengo yake, MSD inadumisha na kusimamia mfumo wenye tija wa ununuzi, utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya vya umma nchini na baadhi ya binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya. 

Alitaja kazi nyingine ni kutumia ujuzi, weledi, mbinu, taratibu na ushauri wa kitaalamu katika kusimamia na kudhibiti utunzaji na usambazaji wa bidhaa za afya. 

Alitaja eneo lingine ni kufuatilia mahitaji ya bidhaa za afya na kusimamia usambazaji wake katika vituo vya kutolea huduma za afya, huduma za afya katika vituo vya umma na kuboresha pale inapobidi na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za afya zinapatikana kwa wakati. 

Sipendi aliongeza kuwa ili kuhakikisha hayo  yote yanafanikiwa, MSD imefanya maboresho kwa kukasimu  baadhi ya madaraka na majukumu kwa kanda ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu katika eneo hilo.

Aidha, MSD imeanza kusambaza bidhaa za afya mara sita kutoka mara nne ya awali na kuwezesha kuboresha mifumo ya ndani ya utendaji, kuboresha huduma na mawasiliano na wateja.

Alisema kutokana na serikali kutenga na kuleta fedha za kununulia bidhaa za afya kama ilivyopanga, upatikanaji wa bidhaa za afya umepanda kutoka asilimia 54 iliyokuwepo mwishoni mwa mwaka jana na kufikia asilimia 76 sasa, kuongeza wataalamu ili kuweza kuwa na fani mbalimbali kuendana na majukumu ya MSD.

Pia Sipendi alisema MSD imeweza kufanikisha kusambaza vifaa vya uzazi pingamizi wa mama na mtoto (CEmONC), vifaa vya maabara na mashine za kusafisha damu kwa baadhi ya hospitali kama vile Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dk.Mganga alisema mkutano huo umelenga kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba na kujadili changamoto  zinazovikabili vituo vya afya vya kutolea huduma ili ziweze kupangiwa maazimio na mikakati ambayo itamsaidia mteja au mwananchi kupata huduma iliyo bora. 

“Mheshimiwa Rais wetu Dk.Samia Suluhu Hassan ametoa kipaumbele kikubwa katika sekta ya afya kwa kutoa fedha nyingi za kujenga Hospitali za  Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati , tumejenga majengo ya wagonjwa mahututi (ICU) majengo ya kupata huduma ya dharura ambayo ni ya kisasa,” alisema Dk.Mganga.

Alisema Serikali imefanya yote hayo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora na za uhakika.

Aidha, Dk.Mganga  alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Samia kwa kufanya kipengele chake na kilichobakia ni kwa wadau, MSD na wafanyakazi kuboresha pale ambapo amekomea na wanalojukumu la kuhakikisha mgonjwa anapata matibabu bora.

Aliongeza kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi  wanapoambiwa dawa hakuna na jambo ambalo linatokana na madaktari kukalili dawa aina moja wakati magonjwa yaliyo mengi yanatibiwa zaidi ya dawa moja.

"Dawa inaweza kutolewa kama mbadala na kuondoa dhana ya wananchi kuichukia Serikali yao pale wanapoambiwa dawa hakuna, madaktari nawaomba  kabla ya kumuandikia mgonjwa dawa mjue akiba za dawa zilizopo ili kuondoa malalamiko ya wananchi.

Kwa  upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Victorina Ludovick alisema maagizo yaliyotolewa na Katibu Tawala Mkoa yatafaniwa kazi ikiwamo uboreshaji wa huduma za afya pamoja na upatikanaji wa bidhaa za afya.

Meneja wa MSD Kanda ya Kati, John Sipendi, akizungumza kwenye mkutano huo.

Mfamasia wa Mkoa wa Singida, Elikana Lubango akitoa wasilisho la wateja wa MSD.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itigi Emmanuel Mallange ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo.
Mfamasia wa Kanda na Afisa Huduma kwa Wateja MSD Kanda ya Kati Dodoma, Michael Mwakuna akichangia jambo kwenye mkutano huo ambapo aliomba wateja wa MSD wawe wanatoa oda siku 10 kabla ili waweze kupata mahitaji yao ya dawa na bidhaa zingine mapema.
Msimamizi wa Huduma za maabara Kanda ya Kati MSD, Omari Hemed Khamis akichangia jambo kwenye mkutano huo
Meneja wa Maabara Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida, Julius Mwita akizungumza kwenye mkutano huo.
Afisa Mauzo Kanda ya MSD, Dodoma, Innocent Masha akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Wadau wa MSD wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Washiriki wakiwa kwenye mkutano huo.
Mkutano ukiendelea.
Picha ya pamoja na viongozi katika mkutanohuo.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja. Kutoka kulia waliosimama ni Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Ferdnand Katimwa, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Dorisila John, Mganga Mkuu Wiaya ya Ikungi, Solomon Michael, Mganga Mkuu Wilaya ya Iramba, Hussein Sepoko, Mganga Mkuu Wilaya ya Itigi, Emmanuel Mallange, Kaimu Mganga Mkuu Singida Manispaa, Yona Yuna Hamisi na Mganga Mkuu Singida DC, Grace Tongwisangu. 

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: