WAZIRI wa Maji Mhe. Jumaa Aweso leo Mei 5, 2023 amekagua maendeleo na kupokea mabomba kwa ajili ya mradi wa maji Nzuguni.


Mhe. Aweso amesema mradi huu ni wa haraka na utendaji wake ni wa tofauti na fedha zake zitoke kwa haraka kwani wananchi wanataka maji.

“Utoaji fedha za utekelezaji mradi huu uwe wa dharura, kusiwepo kisingizio chochote na mkandarasi akiwasilisha cheti, malipo yafanyike kwa wakati, ili asiwe na kisingizio maana huu ni mradi wa haraka.” Amesema Mhe. Aweso

Amefafanua kuwa kwakuwa mabomba yamefika ni vyema kisiwepo kisingizio cha mkandarasi kukosa fedha ili mradi ukamilike kwa wakati uliopangwa.

Aidha, alimwagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph ahakikishe vifaa vinafika kwa wakati ili mabomba hayo yasambazwe na wananchi wapate huduma ya maji haraka.

Vilevile, aliishauri timu ya mabonde kufanya utafiti wa ziada ili kupata mengine yenye maji ya kutosha ili visima viongezwe na wananchi wapate huduma hiyo kwa urahisi.

Aweso alisisitiza kuwa katika kipindi chote cha utekekezaji wa mradi wizara itasimamia ili wananchi wapate maji na atakua mguu kwa mguu kufuatilia hilo.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Nadhifa Kemikimba amesema watahakikisha fedha zinatolewa kwa wakati mara baada ya mkandarasi kupeleka malipo anayotakiwa kupewa.

Mkurugenzi Mkuu DUWASA Mhandisi Joseph amesema utekelezaji wa mradi huo katika Kata ya Nzuguni utakaonufaisha wakazi 37,929 unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.

Amefafanua kuwa mradi huo wenye mikataba minne yenye thamani ya sh. Bilioni 4.8 ambapo hadi sasa DUWASA imepokea sh. milioni 346.6 kati ya sh. bilioni 1.8 za malipo ya awali ya mradi na kwamba fedha zote zimepokelewa na zimelipa wakandarasi wa awali akiwemo wa ujenzi wa tenki.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya, Charles Mamba aliipongeza serikali kwa kutoa fedha na DUWASA kwa kutekeleza miradi ya maji ili kupunguza mgao wa maji.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bodi DUWASA, Profesa David Mwafupe, amemuhakikishia mhe. Waziri kuwa watakuwa begakwa bega na DUWASA kuhakikisha mradi unakamilika.

Share To:

Post A Comment: