Na John Walter-Manyara

Mradi wa ujenzi wa bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani,  Tanga unaendelea kushika kasi ambapo waguswa 475 mkoani Manyara mpaka sasa wamelipwa fidia kiasi cha shilingi Bilioni 2.3. 

Akizungumza kwenye kikao cha tathmini kuhusu mradi huo mkubwa unaopita pia katika mkoa wa Manyara wilaya za Hanang, Kiteto na Simanjiro, Mwakilishi kutoka Wizara ya Nishati Yovin Uisso amesema kwa sasa kinachoendelea ni kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha mradi huo na kuandaa vituo vikubwa na vidogo vitakavyotumika kwenye ujenzi.

Mratibu wa tathmini na malipo EACOP Mussa Mlupilo amesema waguswa katika mradio huo ni 9,508 na hadi sasa zoezi la kutia saini limefika asilimia 98  huku mkoa wa Manyara kwenye wilaya tatu ikiwa na waguswa 475, ambapo kati yao 462 wametia Saini.

Zoezi linaloendelea ni kutoa notisi watu kuhama ambapo mwisho wa kuhama kwa watu wote ni Mei 6,2023.

Mradi huo utapita katika Mikoa 8 ambazo ni  Kagera, Manyara, Geita, Shinyanga, Dodoma, Singida, Tanga, Tabora katika Wilaya 24.

Katibu tawala mkoa wa Manyara Karolina Mthapula, amesema wataendelea kufuatilia migogoro iliyopo kwenye maeneo ambayo mradi huo utapita ili kuondoa usumbufu wowote unaoweza kujitokeza na kuchelewesha mchakato wa ujenzi wa bomba hilo.

Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima,  Uganda hadi Chongoleani, Tanga kwa upande wa Tanzania  litakuwa na urefu wa kilomita 1,147 ambapo inatarajiwa kuzalisha ajira elfu 10 hadi elfu 15 kwa Watanzania.

Hadi kukamilika kwake, mradi huo unatarajiwa kugharimu dola za Kimarekani bilioni 5.1.


Share To:

Post A Comment: