Na John Walter-Manyara

Naibu waziri wa Katiba na Sheria Paulina Gekul amewataka wanasheria na wasaidizi wa sheria kutumia uwezo wao na maarifa waliyonayo kuwasaidia wahanga wa vitendo vya ukatili na wahitaji wengine kupata haki zao.

Ametoa agizo hilo wakati akifungua mafunzo maalum kwa Mawakili na wasaidizi wa kisheria mjini Babati ikiwa ni mwendelezo wa  Kampeni ya Mama Samia Legal Aid  yenye lengo la kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu masuala ya kisheria na haki za binadamu lakini pia ukatili wa kijinsia.

Amesema vitendo vingi vya ukatili vinafanyika na kesi zake kumalizwa kinyumbani jambo ambalo sio sawa kwa kuwa walitendewa ukatili ndio wanaoumia hivyo jamii ikielewa itabadilika na tabia hizo kukoma.

Amesema Wizara ya Katiba na Sheria imekusudia kuwafikia wananchi wote kuwapatia ushauri wa kisheria na kuzitafutia ufumbuzi wa kisheria changamoto zinazowakabili hatua ambayo itasaidia kuondoa migogoro iliyopo katika jamii.

Mama Samia Legal Aid Campaign ni kampeni inayotekelezwa na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Rais-Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora Zanzibar kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa Serikali na wasio wa Serikali imelenga kuimarisha mfumo wa utoaji haki ambapo kupitia kampeni hiyo wananchi wengi nchini watapewa elimu ya sheria na wenye mgogoro mbalimbali inayohusu ardhi, unyanyasaji wa kijinsia, ndoa, mirathi watapewa huduma ya msaada wa kisheria.


Share To:

Post A Comment: