WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeahidi kutekeleza ombi la Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson la kutoa mafunzo maalumu ya uandishi wa habari za kina kwa wanahabari wa Mkoa Mbeya.

Dk Akson ametoa ombi hilo baada ya taarifa ya majaji waliopitia kazi za waandishi wa habari walioshiriki Tuzo za Tulia za Uandishi wa Habari Mbeya (Tulia Journalism Awards 2022) zilizoandaliwa na taasisi yake ya Tulia Trust kuonesha kazi nyingi hususani za magazeti zilitupwa kwa kuwa hazikuwa na vigezo vya kuingia katika tuzo hizo zilizotolewa kwa mara ya kwanza juzi, jijini Mbeya.

“Naomba Waziri wa Habari Nape Nnauye atusaidie kufadhili mafunzo haya na naomba ashirikiane na timu ya majaji kuwakochi wanahabari wa Mbeya, ili mapungufu yalitokana na vigezo  vilivyowekwa katika tuzo hii wayafanyie kazi na ushiriki wao katika tuzo zitakazotolewa mwakani uwe wa ushindani kwelikweli,” Dk Ackson ambaye pia ni mbunge wa Mbeya Mjini alisema.

Katika kuziimarisha, kuzikuza na kuziboresha tuzo hizo Spika huyo alisema taasisi yake inafikiria kuzifanya ziwe za kitaifa badala ya mkoa wa Mbeya pekee kama ilivyofanyika sasa, ili zishirikishe waandishi wa nchi nzima na kuleta matokeo makubwa katika kukuza tasnia hiyo.

“Kwa kuwa tunataka kuzifanya tuzo hizi ziwe endelevu, kwa kuzingatia ushauri wa majaji tutaangilia uwezekano wa kuziboresha zaidi ili zishirikishe mikoa yote,” alisema huku akiahidi kuboresha zawadi zitakazotolewa kwa washindi ambazo kwa mwaka huu mbali na ngao na vyeti, mshindi  wa kwanza katika kila eneo la ushindani alipata Sh Milioni moja, wa pili Sh 500,000 na wa tatu Sh 300,000.

Wakati waandishi wa magazeti kazi zao zilikosa vigezo, wale wa redio, televisheni na televisheni za mtandaoni kazi zao zilishindanishwa kwenye uandishi wa masuala ya elimu, afya, mazingira, makundi maalumu, utalii na maliasili, utamaduni na michezo, siasa, watoto, habari za uchunguzi, uchumi na biashara, unyanyasaji wa kijinsia na picha bora.

Awali Jaji Mkuu wa tuzo hizo, Rose Haji Mwalimu alisema kazi 39 tu ziliwasilishwa katika kinyang’anyiro cha shindano hilo ambazo kati yake 24 zilikuwa za redio, tisa za tv mtandao na sita za magazeti.

Wakati washiriki wa redio na TV mtandao angalau kazi zao zilionekana zina ushindani katika vigezo tisa vinavyozingatia uandishi wa kina na utafiti, wale wa magazeti kazi zao zilikuwa za matukio zisizo na ubunifu, juhudi za mwandishi, ukamilifu, uchambuzi na upekee katika maeneo yaliyoshindaniwa na hivyo kupoteza sifa.

Akikubali ombi la Spika, Waziri Nape alisema; “Kwa vigezo vilovyowekwa na kwa uwezo wa Tulia Trust, mimi kama waziri nakubaliana na tuzo hizi na nakubaliana pia na wazo la kuzifanya ziwe za nchi nzima.”

Nnauye alisema wizara yake iko tayari kufadhili mafunzo kwa wanahabari wa Mbeya na mbali na kuleta wakufunzi itawashirikisha pia majaji.

Wakati huo huo waziri huyo ameahidi wizara yake kuchangia zaidi ya Sh Milioni 35 kwa Vicoba ya Klabu ya Waandishi wa Habari Mbeya (MPC) ili iwe na Sh Milioni 100 ambayo baada ya kupokea mchango wa Sh Milioni 15 za Dk Tulia umeifanya iwe na mzunguko wa Sh Milioni 65.

“Mbali na kuboresha sheria na sera za habari, mwaka 2023 tunataka uwe mwaka wa uchumi kwa tasnia hii ili uchochee maendeleo yao na Taifa, lakini pia kuzidisha umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania,” alisema na kuongeza kwamba wanaanza na Mbeya ili iwe mfano kwa nchi nzima.

Share To:

Post A Comment: