MAKAMU wa Rais, Dk Philip Mpango anatarajiwa kuwaongoza wananchi wa Jiji la Dodoma kupanda miti ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 59 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira. Dk Selemani Jafo amesema hayo leo Januari 9, 2023 jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar yatakayofanyika Januari 12, 2023.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Jafo amesema Dk Mpango ataongoza maeneo ya Barabara ya Dodoma – Dar es Salaam, kuanzia Stendi Kuu ya Dodoma (Nane nane) hadi Ihumwa pamoja na Shule ya Msingi Msalato.

Amesema shughuli hiyo itatanguliwa na shughuli nyingine za upandaji miti Januari 10, 2023 katika maeneo ya pembezoni mwa barabara ya Dodoma – Dar es Salaam kuanzia chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) hadi Kilimo Kwanza ambayo itaongozwa na Waziri Dk Jafo.

Ameongeza kuwa Januari 11, 2023 upandaji miti utaongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk Pindi Chana katika Bwawa la Swaswa wakati Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Sinyamule ataongoza eneo la wazi la Chidachi.

“Mtakumbuka kuwa serikali ilielekeza mwaka huu wa 2023 hakutakuwa na sherehe kubwa za maadhimisho ya Mapinduzi, katika Uwanja wa Amani kama ilivyozoeleka, badala yake gharama zilizopangwa kuadhimisha sherehe hizo zitaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira imeazimia kuadhimisha sherehe hizo kwa kuendeleza shughuli ya upandaji miti katika viunga na maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma,” amefafanua

Share To:

Post A Comment: