Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila alipokagua moja ya daraja la ndani la watembea kwa miguu katika kijiji cha Makere wilayani Kasulu.
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amezungumzia
umuhimu wa wananchi wa mkoa wa Kigoma kutumia fursa ya ujenzi wa
miundombinu ikiwemo barabara za lami kufanyakazi kwa bidii na kukuza
uchumi.

Amesema ujenzi wa barabara za lami, meli katika ziwa Tanganyika, reli ya
kisasa (SGR) na uboreshaji wa uwanja wa ndege ni dhamira ya Serikali
kuunganisha mkoa huo na dunia, hivyo ni vema wananchi wakatumia fursa
hizo kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kupata maendeleo.

“Takriban KM 400 za lami zinajengwa Kigoma lengo la Serikali ya awamu
ya sita ni kuhakikisha huduma za usafiri na uchukuzi kwa nyanja zote
zinaimarika nchini kote ili kuibua fursa zote za uchumi ikiwemo kilimo na
biashara”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa
barabara ya Kibondo-Mabamba KM 47.9, Waziri huyo wa Ujenzi
amewahakikishia wakazi wote watakaoguswa na mradi huo watalipwa fidia
kwa mujibu wa sheria.

“Hatutamwonea mtu, kwa vile fidia ni jambo la kisheria wote watakaostahili
kulipwa watalipwa”, amesisitiza Prof Mbarawa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng.
Rogatus Mativila amesema barabara hiyo ya Kibondo-Mabamba yenye
urefu wa KM 47.9 inaunganisha mkoa wa Kigoma na mikoa ya Kagera,
Geita na nchi ya Burundi kupitia Gitega hivyo kukamilika kwa ke kwa lami
kutachochea biashara katika ukanda wa magharibi.

Amesema mkandarasi aliyeshinda ujenzi wa barabara hiyo ni kampuni ya
CHICO kutoka China na ujenzi wake utatumia miezi 24 ambapo takriban
shilingi bilioni 63.7 zitatumika.

Naye Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye ameishukuru
Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu unaofanyika Kigoma na

kuahidi kuhamasisha wananchi kulinda miundombinu hiyo ili idumu kwa
muda uliokusudiwa na kutumia fursa ya uwepo wake kupunguza umaskini.
Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya
Nduta-Kibondo-Kabingo KM 62.5 na kumtaka mkandarasi CHICO
anayejenga barabara hiyo kuongeza kasi.


Muonekano wa barabara ya Nduta-Kibondo-Kabingo KM 62.5 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Kigoma.Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa na Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye wakishuhudia utiaji saini wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Kibondo Mabamba Km 47.9, kati ya Mtendaji mkuu wa TANROADS na Mwakilishi wa Kampuni ya CHICO, mkoani Kigoma.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo katika hafla ya utiaji saini wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Kibondo-Mabamba Km 47.9.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye akielezea namna ujenzi wa miundombinu unavyofanyika mkoani humo wakati wa hafla ya utiaji saini wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Kibondo-Mabamba Km 47.9, kati ya Mtendaji mkuu wa TANROADS na Mwakilishi wa Kampuni ya CHICO, mkoani Kigoma
Share To:

Post A Comment: