Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC Captain Mussa Mandia akizungumza wakati wa ziara ya bodi hiyo ilipotembelea ujenzi wa mradi mkubwa wa gati mbili za kisasa katika Bandari ya Tanga ambao kwa sasa unaendelea na utakapokamilika utawezesha meli kutia nanga moja kwa moja gatini.


Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha akizungumza wakati wa ziara hiyo
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC Captain Mussa Mandia  wa pili kutoka kushoto akiwa na Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha(mwenyesuti nyeusi) wakipata maelezo
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TASAC Captain Mussa Mandia katikati akiwa Bandari ya Tanga wakati wa ziara hiyo
Ujenzi ukiendelea kama inavyoonekana

NA OSCAR ASSENGA, TANGA.

MWENYEKITI  wa Bodi ya  Wakurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania  (TASAC) Captain Mussa Mandia ameishauri Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuangalia uwezekano wa kurasimisha Bandari bubu zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini ili kurahisisha utoaji wa huduma. 

 Captain Mandia aliyasema hayo leo wakati wa ziara ya bodi hiyo ilipotembelea ujenzi wa mradi mkubwa wa gati mbili za kisasa katika Bandari ya Tanga ambao kwa sasa unaendelea na utakapokamilika utawezesha meli kutia nanga moja kwa moja gatini.

 Alisema urasimishaji wa Bandari hizo utasaidia kuongeza mapato kwa Halmashauri za maeneo husika lakini pia Bandari yenyewe kuweza kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato

 “Kwa kweli hili la urasimishaji wa Bandari Bubu utasaidia kuongeza mapato ya Halmashauri za maeneo husika lakini pia kuwezesha TPA kuweza kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato”Alisema

 Akizungumzia kuhusu upanuzi wa bandari ya Tanga Captain Mandia amesema kukamilika kwa ujenzi wa gati la kisasa katika bandari ya Tanga kutasaidia kuongeza ufanisi na usalama kwenye bandari hiyo.

"Tumekuja kutembelea bandari za Tanga siyo ya Tanga bali za Tanga kwamaana ya bandari kubwa na bandari ndogo kama mnavyojua Tanga kulikuwa na bandari bubu nyingi na tuliwahi kutoa maelekezo siku za nyuma kwa wenzetu wa TPA warasimishe bandari ili wapunguze kwa manufaa ya Taifa,  "

 Captain Mandia alisema pia suala la ulinzi na usalama limeanzia kwenye bandari kubwa ya Tanga ambayo kihistoria ilianza kujengwa kwa mara ya kwanza mwaka 1888 na kuisha mwaka 1891 ambapo hivi sasa wanashuhudia kazi inatoendelea ya uboreshaji wa bandari hiyo kwa lengo la kuimarisha operesheni za bandari hiyo ili kuweza kubeba mizigo mingi zaidi kwa njia ya kiusalama. 

 Mwenyekiti huyo wa bodi alisema kazi yao pia ni kusimamia usalama wa bandari pamoja na utendaji wake ambapo hivi sasa katika bandari ya Tanga panafanyika kazi ya kuongeza kina cha bandari ili kufikia mita 13 kutoka mita tatu zilizokuwepo hapo awali. 

 Captain Mandia alisema uongezwaji wa kina katika bandari hiyo kutasaidia kuruhusu meli kubwa kuingia bandarini kwani hapo awali operesheni zilikuwa zinafanyika katikati ya maji lakini hivi sasa baada ya kazi hiyo ya ujenzi wa gati hilo wanatarajia mpaka mwezi octoba bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa bandarini hapo. 

 Awali akizungumza wakati wa ziara hiyo, Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha alisema ujenzi huo wa gati unakwenda sambamba na masuala ya kiusalama ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kufuatia meli nyingi zitakazotia nanga kwenye bandari hiyo baada ya gati hilo kukamilika. 

Meneja Mrisha alisema mradi huo utakapokamilika utasaidia kuingiza meli kubwa ikiwemo za magari makubwa  ambazo hazijawahi kutia nanga kwenye bandari a Tanga. 

 Meneja huyo alisema hivi sasa bandari ya Tanga inahudumia Tani laki saba kumi na nane na mianne lakini gati hizo mbili zitakapokamilika bandari hiyo itakuwa na, uwezo wa kuhudumia mpaka Tani milioni 3.

 Ujenzi huo wa gati mbili una urefu wa mita 450 na matarajio ni kwamba ifikapo mwezi mei mwaka huu mita 150 zitakuwa zimekamilika na kuanza kupokea meli zisizozidi urefu huo wa 15 na mwezi octoba mita 450 zote zitakuwa zimekamilika. 

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: