OR-TAMISEMI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassani amesema katika mwaka 2020/2021 Serikali ilifanya ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum ambao wamefikia umri wa kwenda shule na kubaini jumla ya watoto 28,968 wenye mahitaji maalum kati ya watoto 59,784 waliochunguzwa na tayari watoto hao wameandikishwa shule.


Akihutubia wananchi katika ziara Maalum aliyoifanya leo tarehe 07 Machi, 2022 katika Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa ikiwa ni ahadi aliyoitoa siku ya kuzaliwa kwake mnamo tarehe 27 Januari, 2022 Mhe. Samia amesema Serikali ilifanya ubainishaji katika kata 3785 sawa na asilimia 95.7 ya kata zote nchini ambazo ni 3956.


Ameendelea kufafanua kuwa Serikali iliamua kufanya ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalum kwa lengo la kuhakikisha watoto wote waliofikisha umri wa kuanza darasa la kwanda wanaandikishwa na kupata fursa ya kupata elimu nchini.


“ Hatutakubali mtoto wa kitanzania akose elimu kwa sababu ya changamoto ya kimaumbile kwa kuwa kila mtoto anahaki ya kupata elimu ili iweze kumsaidia kimaisha na taifa kwa ujumla” amesisitiza Mhe. Samia.


Amesema Serikali itaendelea kutoa fedha kuhakikisha wanajenga mazingira wezeshi kwa watoto wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kupata elimu katika mazingira bora ya kufundisha na kujifunzia nchini.


Aidha amesema kuwa Serikali itaendelea kujenga uelewa kwa jamii, kuhusu utambuzi , uandikishaji na uchukuaji wa hatua stahiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum katika ngazi zote za elimu kupitia makongamano, vyombo vya habari na majukwaa mengine ya kimataifa.

 

Amewaagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa na Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Dkt. Adolf Mkenda kuhakikisha wanaifanyia kazi miongozo hiyo ili watoto wenye mahitaji maalum wanakaa vyema na wanapata fursa zinazotolewa na Serikali katika sekta ya elimu nchini.


Amesema Serikali imeendelea kujenga shule na madarasa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum na jumuishi ambapo Serikali imeshatumia kiasi cha shilingi bilioni 5.49 kwa ajili ya kununua vifaa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika elimu msingi, sekondari na vyuo.


Amesema katika mwaka 2020/2021 Serikali imechapa na kusambaza vitabu vya maandishi yaliyokuzwa kwa masomo yote kuanzia darasa la Kwanza hadi la saba kwa ajili ya wanafunzi wenye uono hafifu au wasioona kabisa.


Aidha amesema kuwa Serikali imetoa zaidi ya shilingi milioni 700 kwa ajili ya uchapaji wa vitabu hivyo kwa masomo ya sanaa, sayansi na biashaa kuanzia kidato cha kwanza a hadi kidato cha nne na itaendelea kwa kidato cha tano na sita miundombinu ya madarasa

Share To:

Post A Comment: