Na Ashrack Miraji

Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amewataka viongozi wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri na Kata kuacha tabia ya kukaa ofisini na badala yake kushuka chini kuwafuata vijana ili kuwaeleza fursa mbalimbali za kimaendeleo zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya kuwainua kiuchumi.

Akizungumza na vijana wa Jimbo la Same Mashariki mkoani Kilimanjaro, Waziri Nanauka alisema viongozi hao wana wajibu wa kuwafikia vijana moja kwa moja kwenye maeneo yao na kuwapatia taarifa sahihi kuhusu fursa za mikopo, mafunzo, ajira na miradi mbalimbali ya kiuchumi inayotolewa na Serikali.

Alisema katika ziara zake tangu ateuliwe kuwa Waziri wa wizara hiyo, amebaini kuwa idadi kubwa ya vijana hawana taarifa za fursa za maendeleo zinazotolewa na Serikali, hali inayosababisha fursa hizo kuwafikia vijana wachache huku wengi wakibaki nyuma kwa kukosa taarifa.


“Nimegundua taarifa nyingi za fursa za vijana hubaki kwa makundi machache. Serikali ya Awamu ya Sita inataka kila kijana, bila kujali itikadi au eneo alipo, apate taarifa na kunufaika na fursa hizi,” alisema Waziri Nanauka.

Aliongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameagiza fursa zote zinazohusu vijana zitolewe kwa uwazi na usawa, huku viongozi wa ngazi zote wakihamasishwa kuhakikisha vijana wanapata elimu ya namna ya kuzitumia fursa hizo kwa maendeleo yao binafsi na Taifa kwa ujumla.


Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango, alisema kundi la vijana ni kubwa kuanzia ngazi ya dunia, Taifa hadi jimbo lake, akieleza kuwa takribani asilimia 64 ya wakazi wa jimbo hilo ni vijana, hivyo linahitaji mikakati madhubuti ya kuwawezesha kiuchumi.

Kilango alisema miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya jimbo hilo imeongeza imani ya vijana kwa Serikali, ikiwemo mradi wa ujenzi wa barabara ya Mkomazi–Kisiwani Same yenye urefu wa kilomita 101 inayojengwa kwa kiwango cha lami, ambayo imefungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa vijana wa eneo hilo.

Naye Waziri Nanauka aliahidi kushughulikia changamoto zilizowasilishwa na vijana, hususan miundombinu ya umwagiliaji, akisema Serikali inaendelea kutenga rasilimali ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji kwa mazao ya kimkakati yanayolimwa na vijana ili kuongeza tija na kipato.

Kwa upande wao, vijana waliohudhuria mkutano huo, wakati wakiwasilisha risala yao kwa Waziri, walisema wanakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya umwagiliaji katika kilimo cha tangawizi kwenye kata za milimani pamoja na kilimo cha mpunga katika kata za tambarare, wakiiomba Serikali kuharakisha upatikanaji wa miradi ya maji kwa ajili ya kilimo.






 

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: