Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa pili kutoka kushoto) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa pikipiki 300 ambazo zitagawiwa kwa Maafisa Ugani wa Sekta ya Mifugo katika Mikoa 25 nchini katika tukio lililofanyika jijini Dodoma leo. Katikati ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki. Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa na wa kwanza kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Antony Mtaka

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango (katikati) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka funguo ya mfano ikiwa ni ishara ya kumkabidhi pikipiki hizo kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wengine katika tukio lililofanyika jijini Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango (wa pili kulia) akiagana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kushoto) muda mfupi baada ya kuzindua pikipiki 300 na kuzikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka( wa kwanza kushoto). Kulia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega.

Pichani ni sehemu ya pikipiki 300 zilizozinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango na kuzikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Anthony Mtaka kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wengine katika tukio lililofanyika jijini Dodoma.
 Na Mbaraka Kambona, Dodoma


MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amekabidhi Pikipiki Mia Tatu (300) kwa Wakuu wa Mikoa 25 ili zikatumiwe na Maafisa Ugani wa sekta ya mifugo waliopo katika Halmashauri kwa lengo la kuwarahisishia kazi ya kuwahudumia wafugaji nchini.

Mhe. Dkt. Mpango alikabidhi pikipiki hizo muda mfupi baada ya kufungua Kikao kazi cha Washauri wa Mifugo na Wakuu wa Idara za Mifugo na Uvuvi kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma kuanzia leo na kesho.

Wakati akikabidhi pikipiki hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Athony Mtaka kwa niaba ya Wakuu wa Mikoa wengine, Dkt. Mpango  alisema kuwa sekta ya mifugo ni moja kati ya sekta za kipaumbele kwa serikali, na ugawaji wa pikipiki hizo kwa maafisa hao ni katika jitihada za serikali kuboresha sekta hiyo ili iweze kuwa na tija kubwa kwa Taifa.

“Serikali inatambua changamoto za sekta hii, napenda kuwahakikishia serikali inaendelea kuzitatua na ndio maana leo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha kununuliwa kwa pikipiki hizi, na tutaendelea kuboresha huduma za ugani ikiwemo kuendelea kutoa elimu ya ufugaji bora kwa wafugaji wetu,” alisema Dkt. Mpango

Aidha, alitumia nafasi hiyo kuwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Miji na Manispaa kutenga fedha kwa ajili ya kutatua changamoto za maafisa ugani katika maeneo yao huku akiwataka maafisa ugani hao kuhakikisha wanazitumia vyema pikipiki hizo ili kuwasaidia wafugaji kufanya ufugaji wenye tija.

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki alisema pamoja na kazi kubwa inayofanyika ya kuboresha sekta hiyo ya mifugo, bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya maafisa ugani na hivyo alimuomba Makamu wa Rais kuona uwezekano wa serikali kutoa kibali cha ajira kwa ajili ya maafisa ugani.

“Mhe. Makamu wa Rais pamoja na uwepo wa teknolojia ya ugani kiganjani, haiondoi uhitaji wa maafisa ugani, uhitaji ni mkubwa, tunaomba serikali iwaajiri maafisa hawa ili waje kusaidia wafugaji wetu huko waliko,”alisema Mhe. Ndaki

Kuhusu pikipiki hizo, Mhe. Ndaki alisema serikali imetumia Shilingi Milioni 864 kununua pikipiki hizo na zitasambazwa kwa mikoa 25 na  Halmashauri 140 zinatarajiwa kufaidika na pikipiki hizo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa alisema kuwa ili kuhakikisha sekta ya mifugo inaendelea kuleta tija kwa wafugaji watahakikisha asilimia 15 inayotakiwa kutengwa na Halmashauri kwa ajili ya kuendeleza sekta hiyo inatengwa na kusimamiwa vizuri zitumike kuendeleza sekta hiyo kama ilivyokusudiwa.
Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: