Imeelezwa kuwa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Kimila na Viongozi wa Serikali wana wajibu wa kutoa elimu juu ya umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 2022 ili wananchi waweze kutoa ushirikiano pamoja na kutoa taarifa sahihi zitakazowezesha kufanikisha lengo la zoezi hilo.


Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa wakati akizindua Semina ya Sensa ya Watu na Makazi iliyotolewa kwa viongozi wa Dini na wa Kimila ambayo  imeandaliwa na Taasisi ya Dini ya Kiislamu ya TWARIQA ambapo amesema Sensa hiyo itasaidia upatikanaji wa takwimu sahihi  zitakazosaidia utekelezaji wa Dira ya maendeleo ya taifa.


Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote waliopo ndani ya nchi kwa umri, jinsia,mahali wanapoishi, hali ya elimu, ajira, vizazi, vifo na makazi ambapo misingi hiyo ndiyo inayoweza kuanisha mahitaji halisi ya wananchi yakiwemo makundi yenye uhitaji maalum kama vile watu wenye ulemavu, watoto, wanawake, vijana na wazee.


“Natambua viongozi wa Dini zote na viongozi wa Kimila wana jukumu kubwa la kuwa viungo kati ya serikali na wananchi na ili kudumisha amani kupitia nyumba za ibada kwa kufundisha maadili mema kama vitabu vitakatifu vinavyoelekeza na Nina imani viongozi wote mliokuja Leo mnauwezi wa kuelimisha jamii kutokana na nyazifa zenu,” Amesema Dkt. Kiruswa.


Pia, Dkt. Kiruswa amesema kuwa, umuhimu wa Sensa ni pamoja na serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, kuboresha huduma za kijamii na kutoa viashiria vya maendelo.


 Dkt. Kiruswa amesema takwimu  za Sensa ya Mwaka 2012 zilionesha kuwa  idadi ya watu ni zaidi ya million 44, wanaume wakiwa ni zaidi ya milioni 21 sawa na asilimia 48.7 na wanawake zaidi ya milioni 23 sawa na asilimia 51.3, huku milioni 31 sawa na asilimia 70.1 wanaoishi vijijini na  milioni 13 sawa na asilimia 29.6 wakiishi mijini.

Share To:

Post A Comment: