SERIKALI imetenga shilingi bilioni 55 kwa ajili ya utafiti wa madini nchini, huku Mirerani wilayani Simanjiro, Manyara, ikiwekwa katika mpango maalumu wa kufufua uzalishaji wa Tanzanite kwa kufungua wigo mpya wa utafiti katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 636, sawa na ekari 157,192.

Hatua hiyo inalenga kubaini mwendelezo wa mikondo ya madini ya Tanzanite nje ya Ukuta wa Mirerani, kuongeza uzalishaji na kuwapa wachimbaji uhakika wa maeneo yenye madini badala ya kuendelea kutumia mitaji mikubwa katika uchimbaji wa kubahatisha.

Katika mpango huo, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linatarajiwa kuleta mitambo mikubwa ya uchimbaji itakayosaidia shughuli za utafiti, huku wataalamu wa Tume ya Jiolojia Tanzania (GST) wakishiriki kubaini maeneo yenye viashiria vya uwepo wa Tanzanite.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa utafiti wa mwendelezo wa mkondo wenye madini ya Tanzanite, Waziri wa Madini, Antony Mavunde, alisema Serikali imeamua kutumia sayansi kutatua changamoto ya upatikanaji wa madini ya Tanzanite kwani Mji wa Mirerani umekuwa maarufu Duniani.

Alisema utafiti huo utahusisha maeneo ndani na nje ya Ukuta, kwa kuwa uchunguzi wa awali umeonesha uwezekano wa kuendelea kwa mikondo ya miamba yenye Tanzanite katika maeneo ya nje ya eneo linalozungushiwa ukuta.

"Sayansi inajibiwa kwa sayansi. Tunataka wachimbaji wadogo wajue maeneo yenye madini badala ya kuchimba kwa kubahatisha na kupoteza muda na mitaji yao,” alisema Mavunde.

Alisema matokeo ya utafiti huo yanaweza kuiwezesha Serikali kufungua maeneo mapya ya uchimbaji na kutoa leseni kwa makundi mbalimbali, yakiwemo wanawake na vijana na makundi maalumu ya jinsia zote, ili kuongeza ushiriki wao katika uchumi unaotokana na madini hayo.

Mavunde alisema dhamira ya Serikali si kuongeza uzalishaji pekee, bali kuhakikisha wananchi wanaozunguka maeneo ya uchimbaji wanapata manufaa zaidi kutokana na rasilimali hiyo adimu inayopatikana Tanzania pekee.

Alisema zaidi ya Sh bilioni 55 zimetengwa kwa ajili ya utafiti, huku Mirerani ikiwa miongoni mwa maeneo yaliyopewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake katika uzalishaji wa Tanzanite.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Tanzania, Abrahaman Mwanga, aliyemwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,Mhandisi Yahaya Samamba alisema tathmini ya awali iliyofanywa na wataalamu imebaini maeneo nje ya Ukuta wa Mirerani yenye mikondo inayofanana na maeneo ambayo tayari yanafahamika kwa uchimbaji wa Tanzanite.

Alisema tathmini hiyo ilifanyika baada ya Mavunde kufanya ziara Mirerani na kuagiza wataalamu wa Wizara kwa kushirikiana na wadau wa eneo hilo kuchunguza changamoto za upatikanaji wa madini hayo.

"Utafiti wa awali umeonesha kuna maeneo nje ya ukuta yenye mikondo inayofanana na maeneo ambayo tayari tuna uzoefu nayo katika uchimbaji wa ndani ya ukuta. Ndiyo maana Waziri alielekeza GST kuendelea na utafiti wa kina,” alisema Mwanga.

Alisema iwapo utafiti huo utathibitisha uwepo wa mashapo mapya, utakuwa mwanzo wa kufunguka kwa maeneo mapya ya uchimbaji na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wachimbaji na wananchi wa Mirerani.

Aliongeza kuwa utafiti hautajikita kwenye Tanzanite pekee, bali pia utachunguza uwezekano wa kupatikana kwa madini mengine yakiwemo graphite na dolomite.






Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: