Na. Angela Msimbira MKURANGA


Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) katika kutimiza kauli mbiu yake isemayo TARURA tunakufungulia barabara kufika kusiko fikika imejenga daraja lenye gharama ya shilingi milioni 200 linalounganisha barabara ya Mwanambaya - Mipeko katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Mkoani Pwani.


Akikagua ujenzi wa Daraja hilo leo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe Ummy Mwalimu amesema ameridhishwa na kazi ya ujenzi wa daraja la Mwanambaya – Mipeko na kuwapongeza TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga kwa usimamizi wenye weledi katika ujenzi huo


Amesema kuwa kazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani ni kuhakikisha anaimarisha miundombinu vijijini na mijini ili kuwaondolea wananchi changamoto za miundombinu ya barabara katika maeneo yao.


“Daraja la Mwanambaya –Mipeko ni moja ya madaraja yanayojengwa nchi nzima, kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassani anataka kufanya mapinduzi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara za vijijini”amesisitiza Waziri Ummy


Waziri Ummy amesema kuwa katika kuhakikisha miundombinu ya vijijini serikali imeweza kuongeza bajeti ya TARURA kutoka shilingi milioni 275 hadi kufikia shilingi 275 hadi bilioni 940 kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hivyo amewataka wananchi kutegemea mabadiliko makubwa katika kutatua kero za miundombinu ya barabara nchini .


Naye Meneja wa Tarura Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga Mhandisi Silas Dilliwa amesema kuwa ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 65 ambapo ukamilishwaji wa daraja hilo kutasaidia kupunguza adha ya wananchi hasa katika kipindi cha mvua ambapo wengi wao hushindwa kuvuka katika eneo hilo


Aidha Daraja la Mwanambaya – Mipeko linajengwa na Mkandarasi M/S JONENAC CONSTRUCTION LIMITED na linatarajiwa kukamilka mnamo tarehe 4/03/2022

Share To:

Post A Comment: