
Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, CPA. Ashiraf Abdulkarim,akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uchambuzi na uandaaji wa mpango Mkakati mpya wa miaka mitano 2026-2031 wa Shirika la Masoko ya Kariakoo.
....
Shirika la Masoko ya Kariakoo limeanza rasmi maandalizi ya Mpango Mkakati mpya wa miaka mitano 2026-2031, hatua inayolenga kulifanya soko hilo la kimataifa kutoa huduma bora, kwa wakati na kuzingatia mabadiliko ya teknolojia yanayojitokeza duniani.
Mpango huo unakuja baada ya baada ya mpango wa 2021-2025 kumaliza muda wake wa utekelezaji kwa mafanikio makubwa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi mafunzo ya uchambuzi na uandaaji wa mpango huo, Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko ya Kariakoo, CPA. Ashiraf Abdulkarim , amesema maandalizi ya mpango huo umeshirikisha wadau ikiwemo Ofisi Waziri Mkuu TAMISEMI, Wafanyabiashara wa Kariakoo, Wapangaji na wadau wengine ili kuwa na mpango mkakati bora, uliochukua mawazo ya wengi na unaojibu matamanio ya kila mmoja na hivyo kuwa rahisi katika utekelezaji wake.
CPA Abdulkarim ameongeza kuwa katika kuandaa mpango huo, Shirika litazingatia nyaraka mbalimbali ikiwemo Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025-2050, hotuba ya Rais wakati akifungua Bunge la 13, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa, Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025-2030 pamoja na Sheria na miongozo mbalimbali iliyoanzisha Shirika la Kariakoo.
“Mafunzo haya yatafanyika kwa siku tano na yatakuwa endelevu. Lengo ni kuwa na mpango mkakati bora, unaotekelezeka na unaoweza kupimika kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano ambao utalifanya soko la kariakoo kuwa kinara na linalotoa huduma anuai na sio mazao pekee" amebainisha CPA Abdulkarim.
Amesema mpango huo ukikamilika utalibadilisha soko la Kariakoo kuwa kituo cha kisasa cha biashara, chenye mifumo ya kisasa ya uendeshaji na utoaji huduma.
CPA. Abdulkarim amesema kuwa Kariakoo mpya itakuwa na miundombinu ya kisasa kuanzia maeneo ya maegesho ya magari, mifumo ya kuzima moto, maeneo ya dharura, hewa ya kutosha na mifumo ya kiteknolojia ya uendeshaji. Tunataka kuwahudumia Watanzania katika mazingira bora na ya kisasa.
Kwa upande wake, Meneja wa Mipango na Biashara wa Shirika la Kariakoo, Bi. Mwinga Luhoyo amesema maandalizi ya mpango huo yanahusisha tathmini ya mpango uliopita wa 2021–2025 ili kubaini mafanikio, changamoto na maeneo yanayohitaji maboresho.
Meneja huyo ameongeza kuwa lengo ni kuhakikisha mpango huo unaendana na mikakati ya kitaifa na huku ukilenga kuongeza tija, kuimarisha biashara, na kukuza mchango wa Kariakoo katika uchumi wa taifa.

Mkuu wa wilaya ya Karatu Mhe. Dkt. Lameck Ng'ang'a Karanga amewapongeza Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) na shirika lisilo la serikali AFRICAI kwa kuendelea kutekeleza ujenzi wa miradi Miwili (2) ya maji mmoja ukiwa kata Mbulumbulu na mwingine Kata ya Baray.
Mhe. Dkt Lameck ametoa pongezi hizo leo Desemba 12, 2025 ofisni kwake wakati akipokea taarifa ya maendeleo ya miradi ya maji inayotekelezwa na wadau hao katika vijiji vya Kambi ya simba, Dumbechand, Mbuga Nyekundu pamoja na Geobaj
Aidha serikali imewahakikishia wadau hao kuwapa ushirikiano kwa kutumia Mamlaka zake ikiwemo RUWASA ili huduma ya maji iwafikie wananchi popote walipo na kwa nyakati zote.
Miradi hiyo ilianza Oktoba 2025 na inatarajiwa kumalizika mwishoni kwa mwezi Januari 2026 huku zaidi ya wananchi 2, l000 wanakadiriwa kunufaika na miradi hiyo ambayo itamaliza tatizo la maji katika vijiji hivyo.
Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo amewaasa wahitimu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) kujiepusha na matendo maovu na elimu na maarifa waliyopata yawe tunu na faida kwa Taifa.
Mhe. Dkt Akwilapo ametoa wito huo tarehe 12 Desemba 2025 wakati wa mahafali ya 44 ya Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) yaliyofanyika mkoani Morogoro ambapo jumla ya wahitimu 450 wa fani za Jiomatikia (Upimaji Ardhi), Upangaji Miji na Vijiji na Mifumo ya Taarifa za Kijiografia (GIS) walitunukiwa Astashada na Stashahada katika fani hizo.
Mhe. Dkt Akwilapo amewataka wahitimu hao kukumbuka kuwa utii, nidhamu na tabia njema ni silaha itakayowafanya wapendwe mahali popote.
‘’Tukiwa hapa Morogoro tunakumbuka maneno yaliyoimbwa na mwanamuziki wa hapa hayati Mbaraka Mwinshehe na bendi yake ya Okestra Volcano; alisema “Heshima Kijana tanguliza kwanza mbele, ujeuri mbaya; uzuri si hoja tabia njema ni silaha utapendwa popote” mwisho wa kunukuu, alisema Mhe. Dkt Akwilapo.
Amewataka vijana kutodanganyika na maneno ya eti kuna watu wanaitwa Gen Z ambapo alieleza kuwa, hizo ni propaganda za kujenga hofu na kufifisha juhudi za nchi maskini kujitafutia maendeleo.
“Msidanganywe kuwa eti nyie ni kizazi cha vijana wasio na nidhamu, wapenda fujo, wasiosikiliza wazee wao, viongozi wao, chenye kujiamulia mambo yao bila kufuata sheria, taratibu, miongozo na tamaduni zetu; na mambo mengine ya hovyo’’ amesisitiza Mhe. Dkt Akwilapo.
Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, inasikitisha na kushangaza kuona vijana wa Kitanzania wanasikiliza maelekezo ya watu ambao hawaishi Tanzania na wala hawajawahi kuwaona na kupuuza maelekezo ya Viongozi wao na hata wazazi wao ambao wamewalea mpaka hapo walipoifikia.
Amesema, kuhitimu masomo kunatakiwa kuendane na uzalendo waliojengewa wa kuipenda Tanzania na kusisitiza kuwa waithamini nchi yao.
Mhe. Dkt Akwilapo amewataka kutumia utaalamu walioupata kwa weledi, uadilifu na kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo na kuepuka vitendo vinavyoenda kuhatarisha amani.
Vile vile amewataka kuendelea kujifunza kwani elimu ni bahari, haina mwisho na kuwataka wanaobaki chuoni kuongeza bidii katika masomo, nidhamu na kutunza amani na umoja kwani kesho yao inajengwa na maamuzi ya leo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Bw. Musa Ramadhani Kilakala akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Bw. Adam Malima amesema, migogoro ya ardhi imepungua mkoani humo hasa pale wizara ya ardhi ilipoanzisha Kliniki za Ardhi ambazo amezieleza zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuwafikia wananchi katika maeneo yao.
Akitoa taarifa kwa Mgeni Rasmi, Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro (ARIMO) Charles Saguda amesema chuo hicho kina Mpango Kabambe wa Miaka 20 (2023-2043) unaolenga kuboresha mazingira ya kujifunza na kujifunzia na utendaji wa chuo katika kuwaandaa wataalamu wa sekta ya ardhi.
“Mpango kabambe huu unalenga kuongeza udahili wa wana chuo kutoka 660 hadi 5000, kuongeza watumishi kutoka 58 hadi 310 kuongeza program za mafunzo ya wanafunzi kutoka 2 hadi 7 pamoja na kujenga kampasi mpya katika eneo Mlima Kola mkoani Morogoro’’. Amesema Bw. Saguda
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga,akizungumza wakati akizindua Bodi mpya ya Wakurugenzi wa WRRB) hafla iliyofanyika leo Disemba 12,2025 jijini Dodoma.
.......
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb), amesema Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) imeleta mageuzi makubwa katika Biashara ya mazao nchini katika kipindi cha miaka mitano (2019–2025), hatua iliyoongeza tija kwa wakulima na mapato ya Serikali.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo Disemba 12, 2025 jijini Dodoma wakati akizindua Bodi mpya ya Wakurugenzi wa WRRB alipobainisha kuwa mageuzi hayo yameongeza ufanisi, uwazi na matumizi ya TEHAMA katika minyororo ya biashara ya mazao nchini.
Aidha, kiasi cha mazao yanayopitia mfumo huo kimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 120, kutoka chini ya tani 600,000 hadi zaidi ya tani 1.3 milioni kwa mwaka, huku bei za mazao zikiongezeka kwa wastani wa asilimia 15 hadi 35, na hivyo kuongeza kipato cha maelfu ya wakulima.
Pia amesema kuwa idadi ya maghala yaliyosajiliwa imeongezeka kutoka chini ya 300 hadi zaidi ya 500, huku mapato ya Serikali yakipanda kwa zaidi ya asilimia 140 kutokana na ushuru, kodi na tozo mbalimbali.
Waziri Kapinga ameielekeza Bodi mpya kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanaimarishwa na kupanuliwa zaidi katika kipindi kijacho cha miaka mitano huku akiitaka bodi hiyo Mpya kuongeza ufanisi, uwajibikaji na ushindani katika biashara ya mazao nchini.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, amesema kuwa wizara hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo ili kuboresha huduma za masoko na kuongeza tija kwa wakulima nchini pamoja na kuimarisha uwezo wa wakulima, kukuza ajira na kuunganisha kilimo na viwanda ili kuchochea maendeleo endelevu ya taifa.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu, amebainisha kuwa matumizi ya stakabadhi yameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka, ambapo idadi ya stakabadhi imepanda kutoka 33,100 hadi 53,107 kwa mwaka 2024/2025, hatua inayoonyesha kuongezeka kwa uelewa na mwitikio wa wakulima na wafanyabiashara.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga,akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WRRB), Asangye Bangu,wakati alipowasili kwa ajili ya kuzindua Bodi mpya ya Wakurugenzi wa WRRB) hafla iliyofanyika leo Disemba 12,2025 jijini Dodoma.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga,akizungumza wakati akizindua Bodi mpya ya Wakurugenzi wa WRRB) hafla iliyofanyika leo Disemba 12,2025 jijini Dodoma.

Naibu Waziri Wa Kilimo Mh.David Silinde ,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa WRRB) hafla iliyofanyika leo Disemba 12,2025 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah,akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa WRRB) hafla iliyofanyika leo Disemba 12,2025 jijini Dodoma.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga,akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, wakati wa uzinduzi wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa WRRB) hafla iliyofanyika leo Disemba 12,2025 jijini Dodoma.

Sehemu ya washiriki wakisikiliza hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (hayupo pichani) wakati akizindua Bodi mpya ya Wakurugenzi wa WRRB) hafla iliyofanyika leo Disemba 12,2025 jijini Dodoma.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga,akiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuzindua Bodi mpya ya Wakurugenzi wa WRRB) hafla iliyofanyika leo Disemba 12,2025 jijini Dodoma.
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amemtaka mkandarasi wa ujenzi wa kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kukamilisha ujenzi wa majengo ya kituo cha mafunzo ya Uongezaji thamani madini ya vito kwa kuongeza nguvukazi na kufanya kazi kwa masaa 24 ili kukamilisha ujenzi wa jengo kwa muda mfupi.
Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Desemba 12, 2025 mkoani Arusha wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa kituo hicho ulioanza ujenzi rasmi ambapo katika maelekezo yake amemtaka mkandarasi kuzingatia ujenzi bora wenye kukidhi vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba.
Waziri Mavunde amefafanua kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais.Dkt. Samia Suluhu Hassan inatekeleza mikakati yake kwenye mnyororo mzima wa uongezaji thamani madini ya vito kama Sera ya Madini ya Mwaka 2009 inavyoelekeza.
Sambamba na hapo, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa, kuanza kwa ujenzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia Bunge la 13 jijini Dodoma.
Waziri Mavunde amebainisha kuwa, kukamilika kwa kituo hicho , kutaleta faida mbalimbali ikiwa pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi watakao jiunga kwenye kituo, kuongezeka kwa wataalamu wa uongezaji thamani madini ya vito, kufungua fursa za ajira kwa vijana na wafanyabiashara wa madini , pamoja na kutosafirishwa kwa madini ghafi nje ya nchi hivyo kutachagiza ongezeko la mapato kwa taifa.
Pamoja na mambo mengine, Waziri Mavunde ametoa siku 7 kwa Katibu Mkuu Wizara ya Madini kukutana na wakandarasi ,TGC na Taasisi za serikali kwa ajili ya upatikanaji vibali muhimu vya kuendeleza ujenzi.
Kwa upande wake , Mkuu wa Wilaya Arusha Mhe. Joseph Mkude ameahidi kuendelea kufuatilia maendeleo ya ujenzi ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kama Serikali inavyotaka.
Mkude ameongeza kuwa, kukamilka kwa kituo hicho itakuwa moja ya sehemu ya uwekezaji mkubwa wa serikali husasan kwenye Sekta ya Madini mkoani Arusha.
Awali, akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi, Mkuu wa kituo cha TGC Mhandisi. Ally Maganga ameeleza kuwa, ujenzi wa majengo pacha hayo ya ghorofa 8 utagharimu Tsh Bilioni 33 na kukamilika kwake kutaongeza fursa ya vijana wengi kupata ajira kupitia ujuzi wa uongezaji thamani madini ya vito.
Naye, Meneja Mradi Mhandisi Robert Lubuva ameahidi kuhakikisha kama wakandarasi wataongeza nguvu ya rasilimali watu na vifaa ili mradi uweze kukamilika na kuwahudumia watanzania kwa wakati.
๐ Utaimarisha upatikanaji wa umeme Mbagala na Gongo la Mboto
๐ Majaribio yameanza ; Shukurani kwa Rais Samia kwa uwekezaji mkubwa
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesema kuwa mradi wa upanuzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Kinyerezi 1 Extension umekamilika rasmi, ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa Transfoma yenye uwezo wa MVA 175.
Amesema hatua hii ni muhimu kwa kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Jiji la Dar es Salaam, hususan maeneo ya Mbagala na Gongo la Mboto, ambayo yamekuwa yakikumbwa na changamoto za kukatika kwa umeme kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi.
Mhe. Salome amesema hayo Desemba 11, 2025, wakati wa ziara yake katika vituo vya uzalishaji umeme vya Kinyerezi I, Kinyerezi II, Ubungo I, Ubungo II na Ubungo III akiongeza kuwa mradi tayari umeanza majaribio (testing).
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa. Transfoma zimefungwa, majaribio yanaendelea, na wananchi wa Gongo la Mboto na Mbagala sasa watapata umeme wa uhakika,” Mhe. Salome.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema Shirika linaendelea kuboresha miundombinu yake ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka.
Amebainisha kuwa katika eneo la Kinyerezi kumefungwa Transfoma kubwa ya MVA 175, huku maeneo ya Gongo la Mboto na Mbagala yakiwekewa Transfoma ya MVA 120 ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya umeme.
Amesisitiza kuwa idadi ya watu imekuwa ikiongezeka Jiji la Dar es Salaam, hivyo miundombinu ya umeme lazima iboreshwe mara kwa mara ili kuendana na uhitaji uliopo.
"Lengo la Kinyerezi 1 Extension lilikuwa kuongeza uwezo wa kusambaza umeme unaozalishwa kuwafikia wateja wetu kwa kiwango kinachostahili," amesema Bw. Twange.
✔️ _Dkt. Kiruswa Asisitiza kuwa Huo Ndio Mwelekeo Mpya wa Sekta ya Madini Nchini_
✔️ _Mining For A Brighter Tomorrow-MBT Kuwasha Moto wa Maendeleo: Vijana na Wanawake Wachimbaji Kunyanyuliwa_
✔️ _Serikali Kuendelea Kufyeka Leseni Zisizofanyiwa Kazi Ili Kutoa Nafasi kwa Wachimbaji Wengine_
๐ _Rombo- Kilimanjaro,_
Serikali imeeleza kujivunia hatua kubwa zinazopigwa na Wachimbaji Wadogo nchini, wakiwemo wanaochimba Madini ya Pozzolana pamoja na wakataji wa matofali ya volcano (volcanic blocks) katika Kata ya Holili, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, hatua inayoendelea kuonesha kasi ya ukuaji wa Sekta ya Madini siku hadi siku.
Kauli hiyo imetolewa leo Desemba 11, 2025 na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za uchimbaji wilayani Rombo, ambapo amesisitiza kuwa Sekta ya Madini imekuwa mhimili unaochochea na kuunganisha sekta nyingine kama ujenzi, viwanda, biashara, kilimo, maji na maeneo mengine ya uchumi.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeanzisha Programu ya Mining for A Brighter Tomorrow – MBT yenye lengo la kuwawezesha vijana na wanawake wanaojihusisha na uchimbaji mdogo kwa kuwapatia leseni za uchimbaji pamoja na vifaa vya kisasa ili kuboresha uzalishaji wao na kuongeza tija.
“Programu hii ni sehemu ya dhamira ya Serikali kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapiga hatua na kuwa sehemu pana ya uchumi wa taifa,” amesema Dkt. Kiruswa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kufuta leseni za uchimbaji na utafiti ambazo hazifanyiwi kazi, ili kuhakikisha rasilimali madini zinawanufaisha Watanzania kikamilifu na kuondoa vizuizi vinavyochelewesha maendeleo ya sekta.
Kwa upande, Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Mhe. Raymond Mwangwala amesema kuwa uwepo wa madini ya Pozzolana umesaidia kutangaza Wilaya hiyo sambamba na kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Rombo huku vijana wakinufaika na ajira kupitia uwepo wa madini hayo yatokanayo na volcano na miamba ya volcano inayotumika kutengenezea matofali imara.
Kwa upande wake Afisa Madini Mkazi wa Mkoa Kilimanjaro Mhandisi Abel Madaha ameeleza kuwa makusanyo ya maduhuli kutoka Sekta ya Madini katika Mkoa wa Kilimanjaro yamefikia shilingi bilioni 1.63 kuanzia Julai hadi Novemba 2025, ikiwa ni asilimia 45 ya lengo la mwaka la kukusanya shilingi bilioni 4.2 kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hatua imayoashiria mwitikio mzuri wa wachimbaji na usimamizi madhubuti unaoendelea kufanywa na Wizara ya Madini ili kuhakikisha rasilimali za nchi zinachangia kikamilifu kwenye maendeleo ya taifa.
Pozzolana ni aina ya madini ujenzi yenye asili ya udongo au majivu ya volkano ambayo, ikichanganywa na chokaa na maji, huunda saruji yenye uimara mkubwa na hutumika kwa wingi katika viwanda vya saruji hapa nchini.
Na James K. Mwanamyoto - Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ametembelea Soko la Majengo jijini Dodoma na kukagua maendeleo ya ukarabati wa soko hilo, ambapo amemuelekeza mkandarasi Kampuni ya Azhar Construction kukamilisha ukarabati huo ifikapo Mwezi Februari 2026 ili wafanyabiashara waanze kulitumia.
Katika kuhakikisha maelekezo yake yanatekelezwa, Dkt. Mwigulu amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Dkt. Frederick Sagamiko kufanya makubaliano ya kimaandishi na mkandarasi huyo kuwa, hakutakuwa na nyongeza ya muda wa ukarabati wa soko hilo ifikapo Mwezi Februari, 2026.
“Serikali inataka ukarabati wa Soko ukamilike kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa Jiji la Dodoma, ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya kuendelea kukuza uchumi wa wafanyabiashara,” Dkt. Nchemba amesisitiza.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe akimkaribisha Mhe. Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema kuwa ukarabati wa soko hilo la Majengo unatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC).
Akieleza historia ya soko hilo la Majengo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema kuwa, soko hilo linalokarabatiwa ni la muda mrefu lilojengwa kipindi cha uhuru (1960’s) hivyo lilikuwa chakavu kiasi cha kutokidhi mahitaji ya sasa kwa muundo wake.
Mhe. Senyamule amefafanua kuwa, ukarabati wa soko hilo ulianza Mwezi Machi 2025 na ukarabati wake unategemewa kukamilika ifikapo Machi 25, 2026, hivyo ofisi yake inaendelea na juhudi za kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati licha ya maendeleo ya utekelezaji wake kutoendana na muda uliopangwa kimkataba.
Naye, mmoja wa wafanyabiashara katika Soko la Majengo, Bw. Abubakari Athuman amemshukuru Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kufanya ukaguzi wa ukarabati katika Soko la Majengo na kumuelekeza mkandarasi akamilishe ukarabati kwa wakati ili waweze kulitumia soko hilo kwani hivi sasa wanafanya biashara katika mazingira ambayo sio rafiki kibiashara.
Kwa upande wake, mfanyabisahara mwingine Bi. Khadija Abdallah amesema kufuatia maelekezo ya Waziri Mkuu Mhe. Dkt. Mwigulu Mchemba, wafanyabiashara wamepata faraja kuwa mkandarasi atakamilisha ukarabati wa soko ili waanze kulitumia, ikizingatiwa kwamba mvua za masika zitaanza muda si mrefu.
Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Haruni Mapesa amewataka Wanafunzi wa Mwaka wa Kwanza wa Chuo hicho kuhakikisha wanafuata Kanuni, Taratibu na Sheria za Chuo kama zilivyo na zinavyoelekezwa.
Prof. Mapesa ameyasema hayo leo wakati akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa kwanza 2025/2026 kwenye kikao kilicholenga kuwakaribisha rasmi wanafunzi hao ambapo pamoja na mambo mengine alielezea historia ya Chuo, Mipango na Maendeleo ya Taasisi kwa Ujumla wake.
Mkuu huyo wa Chuo amewataka Wanafunzi kuwa na nidhamu kwa kufuata sharia na kanuni za ufanyaji wa mitihani, nidhamu katika Mavazi, kuheshimiana baina yao, lakini pia kuwa na nidhamu kwa Wafanyakazi wanaohudumu katika Taasisi hiyo.
Pia Prof. Mapesa amewasihi sana Wanafunzi wa Chuo hicho kujiepusha na matendo maovu ikiwemo kujihusisha na makundi yasiyofaa, kujiepusha na utumiaji wa dawa za kulevya, pamoja na kuhakiksiha changamoto walizonazo wanaziwasilisha sehemu husika ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati badala ya kufanya vurugu.
“ Jukumu lililowaleta Chuoni ni kusoma kwa bidii na kuhakikisha mnafaulu vyema mitihani kwani ndiyo kipimo cha uelewa wa kile ambacho mtakuwa mmefundishwa, lengo likiwa ni kufikia malengo na matarajio mliyojiwekea katika kutimiza ndoto zenu mlizojiwekea katika maisha.”alisisitiza Prof. Mapesa.
Prof. Mapesa amewataka Wanafunzi hao kuzingatia na kuhakikisha wanakuwa na vitambulisho muda wote wanapokuwa Chuoni, kuhakikisha wanakamilisha Usajili, kutunza Mazingira pamoja na Miundombinu mbalimbali iliyopo Chuoni.
Kwa upande wake Rais wa Serikali ya Wanafunzi Magashi Magina amewataka Wanafunzi wenzake kuzingatia yale yote yaliyoelekezwa na Mkuu wa Taasisi, ili kujiepusha na usumbufu usio wa lazima.
Kupitia kikao hicho, Wanafunzi walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali ambayo yalipatiwa majibu na viongozi kupitia kikao hicho,Kikao hicho kimehudhuriwa na Menejimenti ya Chuo, Serikali ya Wanafunzi, Wafanyakazi Waendeshaji na Wanataaluma.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano na Masoko
CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE
11.12.2025
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray akizungumza na Viongozi Chipukizi wakati wa uzinduzi wa Programu ya Mafunzo kwa Viongozi hao Awamu ya Kwanza yaliofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Viongozi Chipukizi wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray (hayupo pichani) wakati akizindua Programu ya Mafunzo kwa Viongozi hao Awamu ya Kwanza yaliofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Viongozi Chipukizi wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray (hayupo pichani) wakati akizindua Programu ya Mafunzo kwa Viongozi hao Awamu ya Kwanza yaliofanyika jijini Dar es Salaam. Wengine ni wageni waalikwa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray (wakwanza kulia) akimsikiliza Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo (hayupo pichani) wakati akitoa maelezo ya awali kuhusu taasisi hiyo kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri huyo kuzindua rasmi Programu ya Mafunzo kwa Viongozi Chipukizi Awamu ya Kwanza yaliofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Viongozi Chipukizi wakifurahia jambo wakati Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray (hayupo pichani) alipokuwa akizindua Programu ya Mafunzo kwa Viongozi hao Awamu ya Kwanza jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray (wapili kutoka kulia) akiwa katika uzinduzi wa Programu ya Mafunzo kwa Viongozi Chipukizi Awamu ya Kwanza yaliofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo. Wengine ni Watendaji wa taasisi hiyo.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray (katikati waliokaaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Viongozi Chipukizi mara baada ya Naibu Waziri huyo kuzindua Programu ya Mafunzo kwa Viongozi hao Awamu ya Kwanza yaliofanyika jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Viongozi Chipukizi wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray (hayupo pichani) wakati akizindua Programu ya Mafunzo kwa Viongozi hao Awamu ya Kwanza yaliofanyika jijini Dar es Salaam. Wengine ni wageni waalikwa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Taasisi ya UONGOZI mara baada ya kuzindua Programu ya Mafunzo kwa Viongozi Chipukizi Awamu ya Kwanza yaliofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo.
Na Veonica Mwafisi-Dar es Salaam
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray ametoa wito kwa Viongozi kuendelea kujifunza siku kwa siku ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia na kitamaduni yatakayowezesha kubuni mikakati mbalimbali ya kuboresha utendaji kwa ustawi wa taifa.
Mhe. Qwaray ameyasema hayo leo tarehe 11 Disemba, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Viongozi Chipukizi kabla ya kuzindua Programu ya Viongozi hao.
Amesema ili mtu aweze kuwa kiongozi mzuri, ni lazima aendelee kujifunza kila siku kwa lengo la kuweza kukabiliana na changamoto za kiuongozi ikiwemo kubuni mbinu mbalimbali za kusimamia mabadiliko ya kimfumo, kiutawala, kiuchumi, kiteknolojia na kitamaduni yanayojitokeza kila siku.
Mhe. Qwaray amewashukuru na kuwapongeza washirika kutoka Finland na HAUS kwa kukubali kushirikiana na Taasisi ya UONGOZI kubuni na kuandaa programu hii maalumu kwa viongozi na taifa kwa ujumla kwani ina umuhimu wa pekee katika kuendeleza viongozi nchini Tanzania na Afrika kwa ujumla.
Aidha, amewasisitiza Viongozi kushirikiana na watumishi walio chini yao kwa kuwaelekeza kazi badala ya kuwaacha na kuwaona ni tatizo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kiongozi usiwe mchoyo kufundisha walio chini yako, tuwafundishe, tunakua, tutengeneze viongozi wa baadae, tusishikilie madaraka, tutengeneze viongozi wengi kadri tuwezavyo, Kiongozi hutakiwi kushikilia kila kitu, shirikisha wenzio ili upate mawazo mapya, kuboresha utendaji na kufikia malengo mahususi yaliyowekwa kwa ustawi wa taifa, Mhe. Qwaray amesisitiza.
Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs 2030), Ajenda ya Maendeleo ya Afrika (Agenda 2063) na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na malengo hayo yameweka bayana kuwa mabadiliko ya kiuongozi ni muhimu kwani ndiyo nguzo kuu ya kufikia malengo yaliyowekwa huku akitolea mfano Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kuwa imeweka malengo ya kuwa na uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
“Ni dhahiri hatuwezi kufikia lengo hili kama tusipojipanga na kuweka mikakati madhubuti ya kutuwezesha kufikia malengo yetu.”
Ametaja moja ya mikakati hiyo ni pamoja na kuwa na nguvu kazi yenye uwezo na motisha pamoja na kuwajengea uwezo viongozi kupitia mafunzo kama haya.
Programu hii ni muhimu sana kwani itasaidia Serikali kuwa na viongozi watakaotimiza matarajio ya wananchi.
“Nina imani kuwa maarifa na ujuzi utakaotolewa kwa washiriki wa programu hii utawapa msingi bora na utayari kuongoza na kutoa huduma bora kwa wanachi.
Mhe. Qwaray amewashauri viongozi kujifanyia tathmini ili kutambua uwezo na udhaifu wao kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kuboresha utendaji hasa kwenye eneo la mapungufu.
Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri kuzindua Programu hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo amesema Taasisi yao imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali ya uongozi ili kuwa na viongozi bora katika taifa.
“Kunaweza kukawa na mifumo mizuri lakini viongozi sio wazuri, hivyo mafunzo tunayoyatoa yanasaidia kuwajenga viongozi kuendana na mifumo mizuri iliyopo, Bw. Kadari ameongeza.






















