Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde amemtaka mkandarasi wa ujenzi wa kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kukamilisha ujenzi wa majengo ya kituo cha mafunzo ya  Uongezaji thamani madini ya vito kwa kuongeza nguvukazi na kufanya kazi kwa masaa 24 ili kukamilisha ujenzi wa jengo kwa muda mfupi.

Waziri Mavunde ameyasema hayo leo Desemba 12, 2025 mkoani Arusha  wakati wa ziara yake ya  kukagua mradi wa kituo hicho  ulioanza ujenzi rasmi ambapo katika maelekezo yake amemtaka mkandarasi kuzingatia ujenzi bora wenye kukidhi vigezo vilivyoainishwa kwenye mkataba.

Waziri Mavunde amefafanua kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais.Dkt. Samia Suluhu Hassan  inatekeleza mikakati yake kwenye mnyororo mzima wa uongezaji thamani madini ya vito kama Sera ya Madini ya Mwaka 2009 inavyoelekeza.

Sambamba na hapo, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa,  kuanza kwa ujenzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Mhe. Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia Bunge la 13 jijini Dodoma.

Waziri Mavunde amebainisha kuwa,  kukamilika kwa  kituo hicho , kutaleta faida mbalimbali ikiwa pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi watakao jiunga kwenye kituo, kuongezeka kwa wataalamu wa uongezaji thamani madini ya vito, kufungua fursa za ajira kwa vijana na wafanyabiashara wa madini , pamoja na kutosafirishwa kwa madini ghafi nje ya nchi hivyo kutachagiza  ongezeko la  mapato kwa taifa.

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mavunde ametoa siku 7 kwa Katibu Mkuu Wizara ya Madini kukutana na wakandarasi ,TGC na Taasisi za serikali kwa ajili ya upatikanaji vibali muhimu vya kuendeleza ujenzi.

Kwa upande wake , Mkuu wa Wilaya Arusha Mhe. Joseph Mkude ameahidi kuendelea kufuatilia maendeleo ya ujenzi ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kama Serikali inavyotaka.

Mkude ameongeza kuwa, kukamilka kwa kituo hicho itakuwa moja ya sehemu ya uwekezaji mkubwa wa serikali  husasan kwenye Sekta ya Madini mkoani Arusha.

Awali, akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi, Mkuu wa kituo cha TGC Mhandisi. Ally Maganga ameeleza kuwa, ujenzi wa majengo pacha hayo ya ghorofa 8 utagharimu Tsh Bilioni 33 na kukamilika kwake kutaongeza fursa ya vijana wengi kupata ajira kupitia ujuzi wa uongezaji thamani madini ya vito.

Naye, Meneja Mradi Mhandisi Robert Lubuva ameahidi kuhakikisha kama wakandarasi wataongeza nguvu ya rasilimali watu na vifaa ili mradi uweze kukamilika na kuwahudumia watanzania kwa wakati.







Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: