Kampuni ya Noble Helium kutoka Australia imetangaza mpango wa kuajiri zaidi ya vijana 50 kupitia utafiti mpya wa Helium unaotarajiwa kuanza mwezi Desemba hadi Februari katika kijiji cha Kinambo, Wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa.

Akizungumza kupitia mahojiano maalum hivi karibuni Mwakilishi wa Kampuni hiyo, Pius Simeon Mwita, alisema Noble Helium imefanikisha tafiti mbalimbali za awali na kubaini viashiria muhimu vya uwepo wa gesi ya Helium, huku ikichangia ajira na maendeleo kwa jamii zinazozunguka maeneo ya uchimbaji.

Mwita alisema katika tafiti zilizopita kampuni ilitoa ajira zisizo rasmi zipatazo 450, na pia ilishirikisha wananchi kwenye utoaji wa huduma kama ulinzi, usambazaji wa bidhaa, vilainishi kwa shughuli za uchorongaji, zabuni ndogo, ununuzi wa chakula pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Aidha, alisema Noble Helium imekamilisha tathmini na ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopo katika maeneo ya leseni ya utafiti wa Helium, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha shughuli za kampuni zinaendeshwa kwa kuzingatia maslahi ya jamii na sheria za nchi.

Kwa mujibu wa Mwita, utafiti mpya utakaofanyika Kinambo utaongeza nafasi nyingine zaidi 50 kwa vijana, na hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika eneo hilo. 

“Tunawaomba vijana wajitokeze kwa wingi pindi fursa hizi zitakapotangazwa. Lengo letu ni kuhakikisha jamii inanufaika moja kwa moja na uwekezaji huu,” alisema.

Utafiti huo unatarajiwa kuongeza kasi ya maandalizi ya uwekezaji mkubwa wa Helium nchini, gesi ambayo imekuwa na mahitaji makubwa duniani kwa matumizi ya teknolojia za tiba, anga na vifaa vya sayansi.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: